Thursday, 23 November 2017

IRINGA VIJIJINI YAENDELEA KUUA MAZALIA YA MBU


MKUU wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela amewaagiza wakazi wa wilaya yake kufukia vidimbwi katika maeneo yao ili kuua mazalia ya mbu, zoezi litakaloipunguzia serikali mzigo wa kutumia fedha nyingi kupambana na ugonjwa wa maralia unaoua maelfu ya watanzania.

Pamoja na kufukia vidimbwi, Kasesela amewataka wananchi hususani wa vijijini kujenga vyoo bora akisema vyoo vya shimo visivyojengwa kwa ustadi mkubwa ni chanzo pia cha mazalia ya mbu.

Aliyasema hayo jana katika kitongoji cha Isakalilo kata ya Tosamaganga wilayani humo alipokuwa akizindua zoezi la matumizi ya viuadudu katika kuangamiza mazalia ya mbu.

“Viongozi wa vitongoji na vijiji, hakikisheni kila eneo hakuna vidimbwi na wananchi wenye bendera nyekundu kwasababu ya kutokuwa na vyoo, wanajenga vyoo bora kabla hatua za kisheria hazijachukuliwa dhidi yao,” alisema.

Awali Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Dk Ignas Mlowe alisema kwa kushirikiana na wahudumu wa ngazi ya jamii, halmashauri hiyo imetambua jumla ya mazalia ya kudumu ya mbu waenezao maralia 316 na imechora ramani kuonesha mahali ambapo mazalia hayo yapo katika kila kitongoji na vijiji 

Alisema mpaka ilipofika Novemba 17, jumla ya madumu 222 kati ya 270 ambayo ni sawa na lita 4,440 za viuadudu zilisambazwa katika vituo vya kutolea huduma kwa ajili ya kuangamiza mazalia ya mbu.

“Kati ya hizo, lita 600 tayari zimeshatumika. Matumizi yanaonekana ni madogo kwa kuwa kipindi hiki hakuna mvua hivyo mazalia yenye viluwiluwi vya mbu ni machache,” alisema.

Ili kufanikisha zoezi hilo, Dk Mlowe alisema halmashauri yao imeviagiza vituo vyote vya kutolea huduma za afya kununua pampu na kusimamia zoezi hilo katika ngazi ya vitongoji na vijiji.

“Jumla ya vituo 55 kati ya 74 tayari vimenunua pampu hizo, na idara ya afya imeagiza pampu 10 kwa ajili ya kusaidia vituo visivyo na uwezo wa kifedha,” alisema.

Aidha alisema halmashauri imetoa mafunzo kwa maafisa afya wa kata 13 na waganga wafawidhi wa vituo 74 ili washirikiane katika kutoa mafunzo kwa wahudumu wa kujitolea ngazi ya vijiji na vitongoji pamoja na kusimamia zoezi zima la upulizaji wa viuadudu katika madimbwi kwenye maeneo yao.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment