Saturday, 11 November 2017

EMANUEL SEDE APIGA HAT TRICK YA KWANZA ROBO FAINALI SPANEST CUP

Image result for Kitisi FC

MAPOGOLO FC wameonesha ubabe katika mechi ya kwanza ya robo fainali ya Kombe la SPANEST Piga Vita Ujangili, Okoa Tembo wakiichapa Mahuninga FC 3-0, mabao yaliyofungwa na Emanuel Sede anayekuwa mshambuliaji wa kwanza kuweka rekodi ya Hat Trick katika ligi hiyo.

Sede, mshambuliaji mwenye kasi na kipaji cha hali ya juu, alifunga magoli hayo katika Dk 52, 60 na 67 yote yakitinga wavuni kutokana na uzembe wa safu ya ulinzi ya Mahuninga.

Kwa ushujaa huo, Emanuel Sede ameondoka na mpira atakaokabidhiwa rasmi katika mchezo wa marudiano utakaopigwa wiki ijayo.

Katika mechi nyingine, magoli mawili ya Omari Panga aliyoyafunga katika Dk 1 na 23 dhidi ya Idodi FC yaliiweka Malizanga FC katika nafasi nzuri ya kutinga nusu fainali endapo itapata sare au ushindi katika mechi yake ya marudiano.

Katika mchezo huo Idodi ilionekana kupigana kufa na kupona, hata hivyo goli lake la kufutia machozi lililofungwa na Enock Kisago katika Dk 14 halikuwazua Malizanga kuondoka na Point 3 muhimu.

Robo fainali ya ligi hiyo inaendelea tena kesho Jumapili, Mboliboli FC ikiikaribishas Itunundu FC huku washindi wa pili wa kombe hilo mwaka jana Kinyika FC wakimkaribisha Ilolompya FC.

Mratibu wa SPANEST, Godwell Ole Meing’ataki amesema mshindi wa kwanza wa kombe hilo atapata seti moja ya jezi, mipira miwili, cheti, medali ya dhahabu, Sh Milioni moja taslimu na safari ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Mshindi wa pili atapata mpira mmoja, cheti, medali ya shaba, na fedha taslimu Sh 700,000 huku mshindi wa tatu akiondoka na mpira mmoja, cheti, medali na fedha taslimu Sh 500,000.

Amesema mshindi wa nne wa mashindano hayo atapata mpira mmoja, cheti, na fedha taslimu Sh 300,000 huku mfungaji bora akiondoka na mpira  mmoja na Sh 100,000 na muazuzi bora akiondoka na jezi na Sh 100,000.

Amesema ligi hiyo inayofanyika kwa mwaka wa nne sasa ilianzishwa na Spanest ambao ni Mradi wa Kuboresha Mtandano wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania ikilenga kuwahamasisha wananchi wa vijiji 24 vya tarafa hizo zinazopakana na hifadhi ya Taifa ya Ruaha kushiriki katika vita dhidi ya ujangili na kuokoa maisha ya Tembo.


“Wanachotakiwa kufanya wananchi hao ni kupiga namba ya simu ya bure 0800751212 na kufichua taarifa za kweli za ujangili, taarifa hizi huwa siri kwahiyo wananchi wasiogope kutoa taarifa hizo,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment