Tuesday, 21 November 2017

CHADEMA YATABIRIWA KUIFUATA NCCR MAGEUZI NA TLP


KADA wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Luciana Mbosa amekifananisha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kilabu kilichoishiwa pombe akisema wateja wake wazuri wameendelea kukikimbia.

Ametoa kauli hiyo baada ya vigogo wake wawili, Lawrance Masha na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha) Patrobas Katambi hii leo kuomba mbele ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kujiunga na CCM sambamba na makada wengine kutoa chama cha ACT wazalendo.

“Kama ilivyokuwa kwa  NCCR Mageuzi, TLP, UDP na vyama vingine vya upinzani kupoteza umaarufu kwa umma na kisha kupotea, anguko hilo sasa linainyemelea Chadema,” alisema katika mkutano wa kumnadi mgombea wa udiwani kata ya Kitwiru kupitia CCM, Baraka Kimata.

Naye Kimata aliwaambia wapiga kura wa mtaa wa Uyole mwisho kwamba akiwa Chadema amejifunza mengi yanayokinzana na demokrasia inayohubiriwa majukwaani hatua iliyomfanya ashuke katika basi lao na kupanda basi lenye injini bora.

“CCM ni chama chenye mfumo mzuri, chenye demokrasia ya kweli na ndio maana kimeweza kuongoza nchi kwa miaka yote tangu Uhuru,” alisema.

Kimata alitaja changamoto kubwa mbili zinazoukabili mtaa wa Uyole, maji na umbali wa shule ya msingi akisema atatumia uwezo wake wote kuzishughulikia mara atakapochaguliwa tena kuwa diwani wa kata hiyo.


“Serikali ya CCM ina mipango mizuri ya kutatua kero ya maji, nina hakika suala hilo litafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo lakini pia vijana wetu wanasoma mbali na maeneo haya wanayoishi, kwahiyo nitaanzisha harakati za ujenzi wa shule mpya ili wawe jirani na shule yao,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment