Wednesday, 15 November 2017

CHADEMA YAPATA PIGO, KATIBU WAKE NYANDA ZA JUU KUSINI ATUA CCM


ALIYEKUWA katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wa chama hicho wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini (Nyasa), Frank Mwaisumbe ametangaza kujiondoa katika chama hicho na amepanga kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati wowote kuanzia sasa.

Mwaisumbe aliyeshika wadhifa huo kwa miaka sita kabla hajauachia kwa hiari yake mwenyewe Januari mwaka huu amesema atajiunga na CCM kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Dk John Magufuli za kufufua uchumi wa nchi.

“Safari yangu ya kisiasa ndani ya Chadema kwa kipindi chote nilichokuwa huko imekoma leo, sasa naona nahitaji kuungana na watanzania wenzangu kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano na kazi zake zote zinazolenga kuleta maendeleo ya Taifa,” alisema.

Akizungumzia tafsiri potofu ya baadhi ya watu wanaoamini kila anayetoka upinzani na kwenda CCM amenunuliwa, Mwaisumbe alisema; “Kwanini CCM waninunue, sina hakika kama CCM wananihitaji kwa kiwango cha kuninunua lakini nisema mimi binafsi ndiyo ninayeihitaji CCM kwahiyo nakwenda kwa hiari yangu mwenyewe.”

Mwaisumbe ambaye kitaaluma ni mchumi alisema ameisoma vizuri Katiba ya CCM na atakapokuwa mwanachama wake, atatimiza wajibu wake kama inavyotakiwa kufanywa na mwananchama mwingine yoyote.

Mwaisumbe ametangaza uamuzi huo leo katika hoteli ya Ambassador mjini Iringa ikiwa ni siku moja tu baada ya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrance Masha kutangaza kurejea CCM baada ya kujiondoa Chadema aliyoitumikia kwa miaka miwili.

Na wakati chama hicho mjini Iringa kikiwa katika maandalizi ya kumpokea Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe anayekuja kuongeza nguvu katika kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Kitwiru.

Wakati Chadema wamemsimamisha Bahati Chengula katika uchaguzi huo, CCM wamemsimamisha Baraka Kimata, diwani wa zamani wa kata hiyo aliyechaguliwa mwaka 2015 kupitia Chadema kabla hajajitoa na kujiunga na CCM hivikaribuni.

Pamoja na pigo hilo Chadema jimbo la Iringa Mjini imepoteza madiwani wengine watatu kwa nyakati tofauti hivikaribuni, wawili wakiwa ni wa viti maalumu na mmoja wa kata ya Kihesa ambao kwa pamoja walijiunga na CCM wakati chama hicho kikizindua kampeni zake udiwani katika kata hiyo, shughuli iliyohudhuriwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi Taifa, Humphrey Polepole.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment