Saturday, 4 November 2017

CHADEMA WAANZA KITWIRU NA SUGU, CCM WAANZA KIMALA NA KIBAJAJI UCHAGUZI MDOGO UDIWANI

Image result for CCM vs Chadema


KIPENGA cha kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata ya Kitwiru Iringa Mjini na Kimala wilayani Kilolo kinapulizwa leo kwa vyama vyenye ushindani mkubwa, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Mapinduzi (CCM) kuanza kupeperusha bendera za kuwanadi wagombea wao.


Wakati makamanda wa Chadema hii leo wataanza kumnadi mgombea wao, Bahati Chengula anayewania udiwani katika kata ya Kitwiru, Iringa Mjini; Vigogo mbalimbali wa CCM watakuwa katika kata ya Kimala wakimnadi mgombea wao wa chama hicho Amon Kikoti.

Katika kinyang’anyiro hicho Chengula anachuana na Baraka Kimata wa CCM na Kikoti anachuana na Tumson Kisoma wa Chadema.

Katika uzinduzi wa kampeni yaa Kimala, CCM itasindikizwa na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (Kibajaji) na viongozi, mbunge wa jimbo la Kilolo Venance Mwamoto na makada mbalimbali wa chama hicho huku katika kata ya Kitwiru, Chadema itamkaribisha Mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi (Sugu) na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche  watakaopanda jukwaani na wabunge wa chama hicho mkoani Iringa, Mchungaji Peter Msigwa na Suzan Mgonakulima.

Uchaguzi huo wa marudio unafanyika baada ya aliyekuwa diwani wa Kitwiru kupitia Chadema, Baraka Kimata kujivua uanachama wa chama hicho na kujiunga na CCM kabla ya hivikaribuni CCM kuonesha imani yake kwake na kumteua tena kuwania nafasi hiyo.


Uchaguzi wa kata ya Kimala unarudiwa baada ya aliyekuwa diwani wa kata hiyo Mejusi Mgeveke kupitia CCM kufariki dunia mapema mwaka huu. Kabla ya kufariki dunia, Mgeveke alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kilolo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment