Tuesday, 14 November 2017

CHADEMA IRINGA MJINI YADAIWA KUPOTEANA, SIRI ZAVUJA


MGOMBEA Udiwani wa kata ya Kitwiru Iringa Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Baraka Kimata amekishukuru chama hicho kwa kumpa nafasi hiyo akisema; “Ni heshima kubwa nitakayoitumia kusukuma maendeleo ya wakazi wa kata hii.”

Kimata amekiri kuzifahamu changamoto mbalimali za maendeleo katika kata hiyo, akisema zitashughulikiwa kwa kupitia utekelezaji wa Ilani ya chama hicho na michango ya wananchi na wadau wengine wa maendeleo.

Ameahidi kutotumia lugha za matusi katika kampeni zake zote tofauti na inavyofanywa na wapinzani wake, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

“Tuwaache watukane, Novemba 26 tuwape adhabu kwa kuwanyima kura,” alisema katika mkutano wake aliofanya mtaa wa Nyamuhanga hivikaribuni.

Alisema taarifa za ndani kutoka katika chama hicho zinaonesha Chadema wanazidi kupoteana, hawana bajeti ya kampeni, hali yao ni mbaya na wanaotaka kuhamia CCM wanatishwa.

“Niwaambie mnaotaka kutoka tokeni mjue kwenye chama kinachounda serikali, na tunawahakikishia ulinzi, yoyote atakayeguswa vyombo vya dola vitafanya kazi yake,” alisema.

Alisema anazo taarifa za uhakika kwamba Kamati Kuu ya chama hicho Iringa mjini haipo pamoja, na baadhi ya madiwani wamesusa kufanya kampeni za mgombea wao, yote hayo wanafanya wakitaka kupeleka ujumbe kwa viongozi wa kitaifa kwamba wamechoka kuburuzwa na Mbunge wa Jimbo la Iringa Mchungaji Peter Msigwa.

“Wote hao wananiombea nishinde uchaguzi huu kwa kishindo ili kutoa fundisho kwa Mchungaji Msigwa ambaye umanifu wake unazidi kuporomoka,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment