Chama cha Mapinduzi kimeendelea kuwaomba
wananchi wa kata ya Kitwiru wamchague mgombea wake, Baraka Kimata kuwa diwani
wa kata hiyo huku kikikanusha tuhuma mbalimbali zinazotolewa na wapinzani wao
dhidi ya mgombea huyo na chama hicho.
Katika mkutano wake ulifanyika mtaa wa
uyole, Diwani wa kata ya Mshindo, Ibrahim Ngwanda amewataka wapiga kura wa kata
hiyo kuupuza madai ya wapinzani wao kwa mgombea wao ambaye awali alikuwa diwani
wa kata hiyo kupitia Chadema, kwamba alinunuliwa kabla ya kuhamia CCM.
“Hatujanunua diwani yoyote wa Chadema na
wala hatuna mpango wa kufanya hivyo. Iliyoko mdarakani ni serikali ya CCM,
Ilani inayotekelezwa ni ya CCM na hata hao wapinzani wanatekeleza Ilani hiyo
hiyo, kwanini tununue wapinzani wanaotekeleza pia Ilani yetu?” aliuliza.
Alisema kama biashara ya kununua
wapinzani ingekuwa inabadili mfumo wa chama hicho na serikali yake katika kutekeleza
majukumu yake, basi mtu wa kwanza kununuliwa mjini Iringa angekuwa Mbunge wa
Jimbo la Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa.
Akiomba kura kwa wapiga kura wa mtaa huo,
Kimata alisema; “Nimeondoka Chadema kwasababu nadhani kuhudumia wananchi
kunahitaji ushirikiano wa chama na viongozi waandamizi mbalimbali, mambo ambayo
niliyakosa nikiwa katika chama hicho.”
Kwasababu ya kukosa ushirikiano toka kwa
Mbunge Msigwa na Meya wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe, aliona haiwezekani tena
kuwatumikia na kuwaletea maendeleo wananchi wa kata hiyo kwa kupitia Chadema.
Anasema ameingia CCM kwasasababu ni chama
ambacho kinajua wapi kinataka kuwapaleka watanzania na kina mfumo unaoeleweka kikatiba
wa namna ya kushughulikia matatizo yake tofauti na Chadema ambako mambo yake mengi
yanashughulikiwa kwa utashi wa mtu au kikundi cha watu.
‘Chadema ni kama gari iliyokosa matairi,
haina injini, akina Mbowe na timu yake ukiwapelekea tatizo walishughulikie, ni watu
wanaongalia nani anayelamikiwa na pale malalamiko yanapohusu watu wao wa jirani
ni wazito kuchukua hatua zitakazoleta muafaka,” alisema.
Alisema amehoji mambo mengi yanayokwenda
ndivyo sivyo ndani ya Chadema hatua iliyopelekea aondolewe katika nafasi yake
ya katibu Mwenezi wa Chadema Jimbo la Iringa Mjini na hatua iliyokuwa ikifuata
dhidi yake ilikuwa ni kufukuzwa uanachama.
“Unawezeje kuendelea kuwa katika chama
kama hicho ambacho kauli ya mtu mmoja au wawili inageuka kuwa maamuzi ya vikao
au maamuzi ya chama?, kwahiyo nikaamua
kuondoka kwa usalama wangu na wananchi wa kata yangu ya Kitwiru,” alisema.
Alimpongeza Rais Dk John Magufuli akisema
anafanya mengi yanayolenga kumkomboa mtanzania na Taifa kwa ujumla hivyo
anapaswa kuungwa mkono.
Akiwaomba kura, Kimata aliwataka wapiga
kura wa kata hiyo wamachague kuwa diwani wao ili aendelee kuyasimamia yale
aliyoyaanzisha na aweze kushughulikia kero zingine za wananchi wa kata hiyo kwa
kutumia Ilani ya CCM inayoendelea kutekelezwa.
0 comments:
Post a Comment