Sunday, 5 November 2017

BABA WA MGOMBEA WA CHADEMA UDIWANI KIMALA, ATAKA MWANAE ANYIMWE KURA

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimezindua kwa kishindo kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata ya Kimala, wilayani Kilolo mkoani Iringa huku Barthromeo Kisoma, baba mzazi wa mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akipanda jukwaani na kuwataka wapiga kura wa kata hiyo wasimchague mwanae.

Wakati CCM inawakilishwa katika uchaguzi huo na Amoni Kikoti mkazi wa kijiji cha Uruti ndani ya kata hiyo, Chadema imemsimamisha Tumson Kisoma anayedaiwa kuhamishia makazi yake Iringa Mjini.

Baba mzazi wa mgombea huyo wa Chadema alitoa rai hiyo baada ya Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Kilolo, Kilian Myenzi kumnyanyua katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni hizo za CCM zilizofanyika jana katika kijiji cha Kimala na kumtaka kuwasalimia wananchi.

“CCM oyee, CCM oyee,” alisema mzazi huyo na kuwafahamisha wananchi waliofurika katika mkutano huo kwamba mgombea wa Chadema ni mwanae lakini hana uwezo wa kuwawakilisha wananchi wa kata hiyo kwa kupitia nafasi hiyo ya udiwani.

Kisoma alisema kata hiyo inahitaji maendeleo ya kweli na mahali pekee pa kuyapata ni kupitia CCM hivyo akawaomba wapiga kura wa kata hiyo wamchague mgombea wa CCM.

Awali Myenzi ambaye pia ni sehemu ya familia ya Kisoma alisema Kata ya Kimala inahitaji diwani wa CCM ili kutengeneza mnyororo utakaorahisisha mawasiliano na serikali ya awamu ya tano ambayo imeundwa na chama hicho.

Akiwaomba wamchague mgombea huyo wa CCM, Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Christopher Magala aliwataka wapiga kura wa kata hiyo kujihadhari na matapeli wa kisiasa wanaobadili rangi za hoja zao kila kukicha.

 “Kabla Rais Magufuli haijaingia madarakani hoja zao zilikuwa rushwa, ufisadi, ubadhilifu wa mali za umma na nyingine nyingi. Baada ya hayo yote kuanza kushughulikiwa katika awamu hii ya uongozi, wamebadilika na sasa  wanatetea watu wanaojihusiha na vitendo hivyo, nchi haihitaji viongozi wa aina hiyo,” alisema.

Kwa upande wake Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa kupitia wilaya ya Mufindi, Jamuhuri William alisema; “sioni ni kwa namna gani, wananchi wa kata hii mtamchagua mgombea kutoka katika chama kilichoshindwa vibaya katika Uchaguzi Mku wa 2015.”

Naye kada maarufu wa chama hicho, Asia Abdalla alisema Kikoti atashinda kwa kishindo katika uchaguzi huo kwasababu wapiga kura wa kata hiyo wanajua mengi yaliyofanywa na yanayoendelea kufanywa na serikali ya Dk John Magufuli.

Abdalla ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kilolo alitaja miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo serikali ya CCM imeitekeleza katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na akasema mengi yanakuja ndani ya awamu ya kwanza ya serikali hiyo.

Akimuombea kura mgombea huyo, Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Venance Mwamoto alisema; “Kikoti ana sifa za kuwa msaidizi wangu kwa kuwa ni mwadilifu, mwaminifu na mchapakazi, hivyo mchagueni yeye.”

Naye Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Zainabu Mwamwindi alisema kata ya Kimala ni kata iliyoongozwa na CCM kwa miaka yote itakuwa miujiza kama watakengeuka.

Akiomba kura kwa wananchi hao, Kikoti alisema atakuwa tayari kutembea kwa miguu kwenda kusikiliza kero mbalimbali za wananchi wa vijiji vya kata hiyo na kuziwasilisha katika mamlaka zinazohusika kwa utatuzi.


“Nitaanzia pale alipoishia diwani aliyetutangulia mbele za haki, nitafanya kazi kwa maarifa na juhudi zangu zote ili kero zilizopo katika kata hii zishughulikiwe ndani ya muda stahiki, uwezo huo ninao” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment