Saturday, 11 November 2017

ASKOFU MDEGELLA ATAKA UBUNGE UWE NA UKOMO AKIZUNGUMZIA MIAKA MIWILI YA DK MAGUFULI

Image result for askofu mdegela

ASKOFU Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Dk Owdernburg Mdegella 
amezungumzia miaka miwili ya serikali ya Dk John Magufuli akimpongeza kwa ujasiri wake wa kushughulikia vitendo vya rushwa ndani ya chama chake.

Akizungumza na wanahabari juzi, Dk Mdegella alisema; “Ndani ya Chama cha Mapinduzi kulikuwa na rushwa kubwa, na hakuna aliyetegemea kama angeweza kuingia kwenye mapambano na wala rushwa ndani ya chama kilichomuweka madarakani.”

Alisema taarifa za rushwa na ufisadi mkubwa zilizokuwa zikitolewa na wanasiasa wa vyama vya upinzani zilikuwa zikielekezwa kwa baadhi ya watu waliokuwa na nafasi kubwa ndani ya serikali na chama hicho.

“Katika vitu ambavyo huwa vinaniamsha usiku kumuombea Rais ni jinsi anavyoendesha mapambano ya rushwa hadi ngazi ya msingi kabisa ya chama hicho ambacho awali rushwa lilikuwa jambo la kawaida hata pale wanapotafutwa viongozi,” alisema.

Alisema mafisadi na wala rushwa wameanza kushika adabu kwasababu wapo waliopelekwa mahakamani na wapo wanaofukuzwa au kunyima nafasi za uongozi ndani ya chama hicho kwa tuhuma tu za kujihusisha na rushwa.

Kwa jinsi kiongozi huyo alivyojitoa kupigania maendeleo ya Taifa lake, Dk Mdegella alisema; “Nilistuka sana nilipoona ameanzisha vita tano kubwa, nikajiuliza ataweza vipi, kwanini asianze na moja na akimaliza aendelee na nyingine?”

Alisema mbali na mapambano ya rushwa ndani ya chama chake, vita nyingine iliyoasisiwa na Dk Magufuli na ambayo imeanza kuzaa matunda ni nidhamu ya watumishi wa umma kazini.

“Huko nyuma kulikuwa na ukichaa wa baadhi ya watumishi kwenda nje ya nchi kufanya vikao vyao wanavyoweza kufanya ndani ya ofisi zao, baadhi ya ofisi zilikuwa zinafungwa bila sababu, wananchi hawapati huduma na mengine mengi ya kuchefua jambo lililofanya wananchi wengi waichukie CCM,” alisema.

Alisema baada ya Dk Magufuli kuingia madarakani na kuanzisha mapambano hayo yaliyokwenda sambamba na kushughulikia tatizo la watumishi hewa na wenye vyeti feki, nidhamu ya watumishi wa umma imeanza kurejea.

Alitaja vita nyingine kuwa ni ile ya kiuchumi akisema kila mahali kwenye upenyo kulikuwa na wizi mkubwa wa rasilimali za umma, na baadhi ya watu waliokuwa wakinyooshewa vidole walikuwa ni wale wenye nafasi nyeti serikalini na ndani ya chama hicho, wizi ambao sasa unashughulikiwa.

“Vita ya nne ni ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya ambayo kwa kiasi kikubwa inaonekana kufanikiwa ikilinganishwa na nchi nyingine zilizoanza mapambano hayo miaka mingi iliyopita,” alisema.

Dk Mdegella alitaja ita ya tano iliyoanzishwa na Dk Magufuli ni ya kunyanyua sekta ya elimu iliyokuwa ikiporomoka siku hadi siku akisema ni vita muhimu hasa kwa Taifa ambalo limejipambanua kutoka hapa lililopo kwenda kwenye uchumi wa viwanda.

Akizungumzia kuhusu katiba mpya alisema kwake yeye hicho sio kipaumbele anachotaka kuona kinafanyiwa kazi na Dk Magufuli kwa sasa, na akawataka watanzania wampe muda kiongozi huyo akamalishe mapambano aliyoyaanzisha na baadae mjadala wa katiba mpya urejeshwe.

“Lakini wakati tukisubiri hilo litokee, muda umefika kwa Taifa kuwa na sheria itakayoweka ukomo wa muda wa uongozi wa mbunge kama kulivyo na ukomo kwa muda wa uongozi wa Rais,” alisema.

Alisema wapo baadhi ya wabunge, wameshika nyadhifa hizo toka utawala wa awamu ya kwanza ya Mwalimu Nyerere na mpaka sasa wanataka kuendelea, hilo sio jambo lenye ustawi kwa demokrasia ya nchi.

“Kuna baadhi ya wabunge , wamekuwa wabunge wakati wa Nyerere, miaka kumi ya Alli Hassan Mwinyi, miaka 10 ya Benjamini Mkapa, miaka 10 ya Jakaya Kikwete, na wanataka wapewe miaka 10 ya Dk Magufuli. Kwa hili tuseme tu ni muhimu nafasi hiyo nayo ikawa na ukomo kama ilivyopendekezwa kwenye rasimu ya Katiba ya Warioba,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment