Sunday, 29 October 2017

WAZALISHAJI ASALI WALIA UKOSEFU WA SOKO
WAKATI serikali ikitaka uzalishaji wa asali uongezwe ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi, kikundi cha Mangalali Farmers Against Poverty (Mfapo)  cha wilayani Iringa kimelalamika kukosa soko la uhakika la bidhaa hiyo.

Taarifa ya ukosefu wa soko la uhakika ilitolewa na mwenyekiti wa Mfapo, Sholla Mgulunde kwa baadhi ya wanachama wa Umoja wa Watanzania waliosoma Japan (JATA) waliotembelea kikundi hicho kujionea shughuli za ujasiriamali wanazozifanya.

Wakiwa na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA) nchini, Kei Umetsu, wanachama hao wa JATA walikuwa wilayani Iringa katika ziara yao ya siku mbili kujionea jinsi shughuli za ujasiriamali wilayani humo zinavyooanishwa na ukuaji wa sekta ya utalii kusini mwa Tanzania.

Akitoa taarifa hiyo, Mgulunde alisema kikundi hicho chenye wanachama 30 kilianzishwa mwaka 2013 huku moja ya lengo lake likiwa ni kutunza sehemu ya msitu wa asili wa kijiji cha Mangalali huku kikifanya shughuli hiyo ya uzalishaji wa asali.

“Tulianza ufugaji wa nyuki tukiwa na mizinga 10 na mwaka jana tukapata ufadhili wa Sh Milioni 26 kutoka Mfuko wa Misitu Tanzania na kuongeza mizinga mingine 250 na hivyo uzalishaji wa asali kuanza kuongezeka,” alisema.

“Awamu ya kwanza ya mavuno tumefanya Julai mwaka huu na tulipata tani tatu za asali, tunatarajia mavuno hayo yataongezeka mara mbili zaidi awamu ya pili ya mavuno tutakayofanya Novemba mwaka huu,” alisema.

Alisema baada ya kuvuna kiasi hicho cha asali yenye thamani ya zaidi ya Sh Milioni 30 hawajui kwa kuipeleka na jitihada zao za kupata soko la uhakika kama inavyoelezwa zimegonga mwamba.

“Katika kukabiliana na changamoto ya soko la uhakika, asali hiyo tumelazimika kuiuza kwa mteja yoyote yule kwa kadri atakavyohitaji,” alisema.

Alisema mauzo hayo hafifu yamedhorotesha mipango yao mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushindwa kushiriki maonesho ya nane nane ya mwaka huu, yanayofanyika kikanda mjini Mbeya kila mwaka mwaka.

“Tunaomba serikali itusaidie kutuunganisha na masoko ya uhakika, uzalishaji wetu unazidi kuongezeka na mwakani tunatarajia kuvuna zaidi ya tani 12,” alisema.


Julai 3, mwaka huu, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tan Trade), Mhandisi Christopher Chizawa alifungua maonesho ya asali katika viwanja vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam akisisitiza uzalishaji uongezwe kwa kuwa masoko ya bidhaa hiyo ndani na nje ya nchi ni makubwa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment