Sunday, 1 October 2017

WATALII WA NDANI WAKIMBILIA HIFADHI YA TAIFA YA RUAHA

WATANZANIA wa kawaida wamejitokeza kwa wingi kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, wilayani Iringa wakiadhimisha maonesho ya Utalii ya Karibu Kusini yanayofanyika kwa mara ya pili mwaka huu mjini Iringa baada ya Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) kutangaza kuratibu safari za utalii katika hifadhi hiyo kwa gharama nafuu.

Jumla ya mabasi manne ya ukubwa wa kati (Coaster); yenye uwezo wa kubeba abiria 25 hadi 30 kila moja, yalifanya safari za utalii katika hifadhi hiyo Septemba 30 na Oktoba 1, mwaka huu ikiwa ni moja ya hatua ya shirika hilo kuhamasisha utalii wa ndani.

“Tulichokifanya Tanapa kinaweza kufanywa kwa gharama nafuu na wadau wengine wa utalii zikiwemo kampuni za kuongoza watalii. Wanachoweza kufanya ni kuratibu na kutangaza safari za aina hii mara kwa mara,” alisema  meneja masoko wa shirika hilo, Victor Ketansi.

Nsanganile John toka Kisarawe, Pwani alisema; “leo ni mara yangu ya kwanza kutembelea hifadhi hii. Nimeona wanyama kama Tembo, Twiga, Swala, Kudu na Simba katika makundi makundi, lakini pia nimeona aina mbalimbali za ndege.”

Alisema amewahi kutembelea hifadhi nyingine mbalimbali nchini, lakini hajawahi kuona wanyamapori wakiwa katika makundi makubwa kama ilivyo ndani ya Hifadhi ya Ruaha.

Pamoja na uzuri wa vivutio katika hifadhi hiyo, John alisema serikali inatakiwa kutengeneza barabara ya Iringa- Ruaha kwa kiwango cha lami ili kuwawezesha watanzania walio wengi kufika kwa kutumia pia magari yao.

Naye Stanley Manyonye toka Shinyanga alisema; “Hii ni mara yangu ya kwanza kufika katika hifadhi hii. Nimeshangaa kwanini ilikuwa haitajwi katika kundi la hifadhi kubwa nchini.”

Alisema hifadhi hiyo kubwa kuliko zote nchini bado haijatangazwa vya kutosha na akawaomba wadau wanaohusika na sekta hiyo kusaidia juhudi za kuitangaza ili ipate watalii wengi zaidi.

Kwa upande wake Silvia kutoka Dodoma alisema; “nimefurahi kupata fursa ya kutembelea Ruaha, tumeona wanyama wengi na tumeburudika kwa kweli.”

Hata hivyo alisema moja ya changamoto waliyoibaini katika hifadhi hiyo na ambayo inatakiwa kufanyiwa kazi ni kukauka kwa Mto Ruaha Mkuu unaopita katika hifadhi hiyo na ambao pia ni chanz cha maji cha wanyama wa hifadhi hiyo.

Pamoja na uzuri wa vivutio vya utalii katika hifadhi, Ashura Sadick toka Kigoma alishauri miti mikubwa ya asili ipandwe ndani ya hifadhi hiyo ili itumike kama kivuli kwa wanyama hao.

“Tumeona miti mingi mikubwa imeangushwa, na maelezo ni kwamba inaangushwa na Tembo wanaotafuta maji wakati wa kiangazi hasa kwa kuwa Mto Ruaha Mkuu umekuwa ukikauka wakati huo. Ipo hatari ya wanyama hawa kwenda nje ya hifadhi hii kutafuta sehemu za kupoza makali ya jua. Kama taratibu zinaruhusu basi ushauri wangu kwa wahusika ni kupanda miti hiyo,” alisema.

Naye Wito Nzombe wa Iringa alisema amefurahi yeye na familia yake kuitembelea hifadhi hiyo kwa mara ya kwanza.

“Ninaishi Iringa jirani kabisa na hifadhi hii; nikiri hii ni mara yangu ya kwanza pia mimi na familia yangu kuitembelea. Nimetumia fursa iliyojitokeza na nitarudia tena itakapotokea tena,” alisema.

Alitoa ushauri kwa watanzania wengine hususani wakazi wa mkoa wa Iringa na mikoa jirani kutembelea hifadhi hiyo kwa makundi ili waweze kumudu gharama za kukodi usafiri wa kuwapeleka.

“Nimekuwa nikiwaona wanyama wa Ruaha na hifadhi zingine kwenye Luninga. Kuna tofauti kubwa kuwaona kwenye Luninga na kuwaona moja kwa moja hifadhini, raha yake haisimuliki kirahisi lakini raha hiyo ni kubwa sana,” alisema.

Nzombe alisema wamefurahi pia kukutana na makundi tofauti ya watalii kutoka nje ya Tanzania wakitalii katika hifadhi hiyo; hakika ina burudani yake.

Maonesho ya Utalii ya Karibu Kusini yameanza mwaka jana na yatakuwa yakifanyika kila mwaka mjini Iringa kwa uratibu wa mikoa ya nyanda za juu kusini kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii,  shirika la kuhudumia viwanda vidogo (Sido) na wadau mbalimbali ukiwemo Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST).

Kwa mwaka huu, maonesho hayo yaliyobeba kauli mbiu ya Utalii ni Nguzo ya Viwanda yamefanyika kati ya Septemba 27 na Oktoba 2, 2017.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment