Sunday, 8 October 2017

WATALII KUTEMBEZWA KWA MIGUU HIFADHI ZA TAIFA NCHINI
ASKARI wanyamapori 88 wa Hifadhi za Taifa mbalimbali nchini wamepata sifa adhimu ya kuwaongoza watalii kufanya utalii wa kutembea kwa miguu hifadhini ili wajionee wanyama na vivutio vingine vya utalii ambavyo si rahisi kufikiwa kwa kutumia magari.

Wamepata sifa hiyo baada ya kufuzu mafunzo hayo yaliyotolewa kwa nyakati tofauti kupitia Mradi wa Kuimarisha Mtandao wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (Spanest) katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Awamu ya nne ya mafunzo hayo yaliyohitimishwa juzi katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha yalikofanyika pia mafunzo ya awamu ya kwanza, ya pili na ya tatu ambayo kwa pamoja yalijumuisha askari 64, ilihusisha askari wanyamapori 24.

Mkufunzi wa mafunzo hayo, Ethan Kinsey alisema pamoja na askari hao kufundishwa jinsi ya kuwaongoza watalii kwa miguu,  hufundishwa pia namna ya kuwaepusha na hatari ya wanyama wakali, kujua tabia za wanyama, kupita vichakani, namna ya kutoa huduma ya kwanza na matumizi ya silaha.

Katika sherehe za kuwatunuku vyeti wahitimu hao 24 wa awamu ya nne, Mratibu wa Spanest, Godwell Ole Meing’ataki alisema; “aina hii ya utalii ni ya upekee kwasababu inawafanya watalii wawe jirani na mazingira na vivutio vyake, tofauti na wanavyotumia magari.”

“Ndani ya hifadhi kuna milima, makorongo, mabonde, vichaka, miti na uwanda wa tambalale, na kuna wanyama na vivutio vingine vingi. Mtalii hawezi kufika katika maeneo hayo kwa kutumia magari kwahiyo lazima apelekwe kwa miguu,” alisema.

Alisema Spanest inayofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF), inatoa mafunzo kwa askari hao ili kusaidia kuboresha shughuli za uhifadhi na utalii, hususani katika hifadhi za kusini.

Akiwatunuku vyeti wahitimu hao, Mkurugenzi wa Mipango wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Dk Ezekiel Dembe alisema Tanzania imechelewa kuanza utalii wa kutembea kwa miguu kwasababu kulikuwepo na ukosefu wa nguvu kazi yenye ujuzi huo na hofu ya kuuawa watalii na wanyama wakali.

“Sasa utalii huo unaweza kufanyika kwasababu tuna majibu; tuna askari wenye mafunzo ya kuongoza watalii, wenye utalaamu wa kutumia silaha zinazotakiwa katika utalii huo na wanaoweza kutoa huduma kwa mgeni pale inapotokea ajali,” alisema huku akiwakaribisha watalii kufurahia aina hiyo ya utalii.

Alisema utalii wa kutembea kwa miguu ni aina ya utalii inayokua kwa kasi kubwa hivyo ni fursa tosha inayoweza kuchangia kukuza sekta ya utalii nchini kama uwezekezaji wake utakuwa wa kutosha.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment