Tuesday, 3 October 2017

WANYAMA WA HIFADHI YA RUAHA HATARINI, MTO RUAHA MKUU WAZIDI KUKAUKA


WATALII wa ndani waliotembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha hivikaribuni wamesikitika kuona samaki wakifa na wanyama wakihangaika kutafuta maji katika bonde la Mto Ruaha Mkuu na wakauliza ilipo mikakati ya serikali ya kuhifadhi na kurudisha ikolojia ya bonde hilo.

Walitembelea hifadhi hiyo kwa uratibu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) wakati wa maadhimisho ya Maonesho ya Utalii ya Karibu Kusini yaliyofanyika kati ya Septemba 29 na Oktoba 2, mwaka huu sambamba na wiki ya Utalii Duniani.

Watalii hao wakaenda mbali wakiwata wanasiasa kuachana na kauli zinazochochea matumizi ya maji yasio endelevu katika maeneo oevu na vyanzo vingine vinavyotiririsha maji katika mto huo ambao ni chanzo pekee cha maji cha uhakika kwa wanyama wa hifadhi hiyo.

Uhaba wa maji katika bonde hilo umezidi kuwa tete ikiwa ni miezi sita tangu Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan aunde kikosi kazi cha kitaifa cha kuhifadhi na kurudisha ikolojia ya bonde hilo.

Alipotembelea bonde hilo ndani ya hifadhi hiyo April 12, mwaka huu, Makamu wa Rais alisema; “nimeona hali halisi ya mto huu, vipimo vya maji vinaonesha viko chini sana na huu ni wakati wa mvua za masika, bila shaka wakati wa kiangazi hali itakuwa mbaya zaidi.”

Kwa kuzingatia hali hiyo alikiagiza kikosi kazi hicho alichokizindua mjini Iringa April 11, mwaka huu, kifanye kazi kwa bidii na maarifa ili kuleta majawabu yatakayonusuru mtiririko wa maji katika bonde hilo.

Baada ya kikosi kazi hicho kuja na majibu, baadhi ya wanasiasa walisikika wakiwapigia debe baadhi ya wananchi wanaofanya shughuli za kilimo, ufugaji na makazi karibu na kwenye vyanzo vya maji yanayotiririka kuelekea katika mto huo wakisema kwa miaka yote maisha yao yamekuwa yakitegema maji kutoka katika vyanzo hivyo.

“Uhai wa wanyama hawa upo wapi kama hakuna maji katika mto huu. Inasikitisha kuona samaki wanakufa na wanaliwa na ndege kwasababu ya kukosa maji,” alisema Ashura Sadick, mtalii wa ndani kutoka Kigoma.

Na inasikitisha kuona wanyama wakubwa wanaovuta watalii wengi kama Tembo, Simba, Twiga na Viboko wakihangaika kwa kukosa maji, alisema.

Wito Nzombe wa Iringa alisema serikali inapaswa kuweka kando siasa kama inataka kuchukua hatua madhubuti kushughulikia tatizo la mtiririko wa maji katika mto huo.

Awali Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Ruaha (Runapa), Dk Christopher Timbuka alisema changamoto kubwa inayoukabili mto Ruaha Mkuu ni matumizi yasio endelevu ya rasilimali maji kwa ajili ya kilimo, ufugaji na makazi yanayofanywa kwenye ardhi oevu ya Ihefu na vyanzo vingine vya maji vinavyotirisha maji katika mto huo.

Alisema kama mto Ruaha Mkuu ambao ni chanzo pekee cha maji katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha utaendelea kukauka kama ulivyokauka hivisasa, hifadhi hiyo itatoweka na hivyo lengo la kuifanya kuwa lango la Utalii kusini halitafanikiwa.

“Tunaendelea na maboresho ya miundombinu ndani ya hifadhi, utangazaji na huduma mbalimbali. Maboresho hayo hayatakuwa na maana kama hali ya mto huo utaendelea kukauka,” alisema huku akiiomba serikali kusaidia kunusuru bonde hilo.

Alisema zimekuwepo jitihada mbalimbali za kunusuru hali hiyo lakini kauli za baadhi ya wanasiasa zinazopinga shughuli za kibinadamu kufanyika kwenye vyanzo vya maji zimekuwa zikikwamisha jitihada za Tanapa na serikali za kumaliza changamoto hizo.

Mbali na changamoto za matumizi ya maji yanayotakiwa kutiririka katika mto huo, Timbuka alisema bado kuna migogoro ya mipaka baina ya hifadhi na jamii katika wilaya za Mbarali na Chunya.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment