Sunday, 15 October 2017

WANAFUNZI WA ZAMANI WAJENGA CHOO CHA MILIONI 30 TOSAMAGANGA SEKONDARI

WANAFUNZI waliosoma katika shule ya sekondari Tosamaganga nje kidogo ya Manispaa ya Iringa, wamejenga shuleni hapo choo cha kisasa chenye thamani ya zaidi ya Sh Milioni 30, mradi walioutekeleza kupitia mfuko maalumu waliouanzisha kwa ajili ya kuboresha mazingira ya shule hiyo.

Kati ya wanafunzi hao, yupo Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga aliyesoma mwaka 1975 hadi 1978, na Protas Ishengoma wa kampuni ya Mawakili ya IMMA, Kaimu Kamisha wa Idara ya Forodha George Mnyitafu na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Pembejeo John Banzi ambao kwa pamoja walisoma kati ya mwaka 1978 na 1980.

Wengine waliosafiri kutoka mikoa mbalimbali na kuja katika shule yao hiyo kushiriki hafla ya makabidhiano ya mradi huo ni pamoja na wahandisi, madaktari wa binadamu, walimu, watafiti, wahasibu, wanajeshi na viongozi wa taasisi za fedha na elimu.

Walikabidhi choo hicho kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Robert Masunya juzi katika hafla iliyokwenda sambamba na shughuli zingine za burudani, michezo na chakula cha pamoja walichokula na jumuiya ya wanafunzi wa shule hiyo.

Akikabidhi msaada huo mbele ya walimu na wanafunzi wa shule hiyo, kiongozi wa wanafunzi hao, Danford Mbilinyi alisema; “Tumeweza kutumia mitandao ya kijamii ya whatsapp na email kurudi nyumbani, wengi wetu kabla ya tukio hili la leo tulikuwa hatufahamiani kwasababu tumesoma miaka tofauti katika shule hii.”

Mbilinyi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Umoja Switch, wasambazaji wa mashine za kutolea huduma za fedha (ATM) katika taasisi mbalimbali za fedha nchini alisema bila shule hiyo huenda wengi wao wasingekuwa na nafasi walizonazo hivisasa katika sekta ya umma na binafsi.

“Kama tunachangia harusi na shughuli zingine za burudani, kwanini tushindwe kuchangia maendeleo ya shule iliyotufanya wengi wetu tuwe hivi tulivyo hivisasa. Tunaendelea kupokea wanachama wapya katika kundi hili na tutaendelea kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo ya shule hii,” alisema.

Baada ya baadhi ya wanafunzi hao kusimulia mafanikio waliyonayo na kuwatia moyo kitaaluma wanafunzi wa shule hiyo ili watimize ndoto zao za maisha yao ya baadaye, Wakili Ishengoma aliuliza; “Kwanini shule hii haina darasa la kompyuta wakati tupo katika ulimwengu wa teknolojia hiyo?”

Baada ya kujenga choo hicho alisema kundi lao litahakikisha linatoa msaada wa kompyuta za kutosha ili shule hiyo iwe na darasa hilo katika kipindi kifupi kijacho.

Akishukuru kwa msaada huo, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo alisema serikali inathamini mchango wa maendeleo unaotolewa na wadau wake kama ilivyofanywa na wanafunzi hao wa zamani wa shule hiyo.

“Mlichofanya ni kumuunga mkono Rais Dk John Magufuli katika harakati zake za kutoa elimu bora kwa watanzania wote na kusukuma maendeleo ya Taifa hili”alisema na kutoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kuchangia sekta mbalimbali za maendeleo.

Wakati huo huo, wanafunzi hao wametoa vifaa tiba yakiwemo mashuka 75 na Sh 200,000 kusaidia kuboresha huduma zinazotolewa katika hospitali teule ya wilaya ya Iringa ya Tosamaganga waliyokuwa wakiitumia kwa matibabu wakati wakisoma sekondari ya Tosamaganga.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment