Sunday, 8 October 2017

WANAFUNZI WA KIKE WA KABILA LA KIMASAI WATIMIZA NDOTO YA ELIMU YA SEKONDARI
WANAFUNZI wa kike 23 wa jamii ya wafugaji wa Kimasai waliokuwa hatarini kukosa elimu ya sekondari kwasababu mbalimbali ikiwemo ya kuozeshwa wakiwa na umri mdogo,  wanatarajia kumaliza kidato cha nne mwaka huu katika shule ya sekondari ya Namnyaki, wilayani Kilolo mkoani Iringa.

Wanafunzi hao wameushukuru mradi wa IMAGE (IMAGE Project) ulioasisiwa na Mmarekani Debra Pangerl kwa kuwawezesha kielimu watoto wa kike wa kabila la Kimasai, wakisema bila ufadhili wao, ndoto yao ya kupata elimu ingeyoyoma kama ilivyotokea kwa dada zao wengi wa kabila hilo.

Mmoja wa wanafunzi hao, Lucia Loseri alisema; “Maisha yangu yote nimelelewa na mama yangu, sikuwahi kumfahamu baba yangu kwani alikufa kabla ya kuzaliwa. Mama alipenda nipate elimu hii lakini hakuwa na uwezo mpaka aliposikia kuna mradi wa IMAGE na kuniombea nafasi.”

Waliyasema hayo juzi wakati shule hiyo iliyopo katika kijiji cha Kilala Kidewa wilayani humo ikifanya mahafali yake ya kwanza ya wanafunzi hao wa kidato cha nne, ikiwa ni miaka minne toka ianzishwe mwaka 2013.

Mkurugenzi wa mradi huo, Debra alisema kwa kushirikiana na baadhi ya watanzania alianzisha mradi huo na baadaye shule hiyo baada ya mwaka 2000 kuhudhuria semina za mafunzo nchini Kenya na Tanzania na kuguswa na simulizi za watoto wa Kimasai waliosema wana kiu ya kupata elimu na kuona sauti zao zinasikika.

“Mradi wa IMAGE ulianza kwa kujifunza mfumo mzima wa maisha ya Masai, mila na tamaduni zao. Tulibaini jinsi watoto wa kike wa Kimasai walivyoishi katika mazingira magumu, tukaamua kuwakomboa kwa kuwapatia elimu na ndipo ikaanzishwa shule hii,” alisema mama huyo wa Kimarekani.

Mbali na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza na Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Asia Abdallah, wengine waliohudhuria mahafali hayo ni pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Iringa na wilaya ya Kilolo na wawakilishi wa mradi wa IMAGE kutoka nchini Marekani.

Mkuu wa shule hiyo Ikupa Mbanga alisema pamoja na kwamba shule hiyo imejengwa wilayani Kilolo mkoani Iringa imekuwa ikichukua wanafunzi wa Kimasai na hata wa makabila mengine waliopo katika mazingira magumu ya kupata elimu kutoka katika mikoa mbalimbali ikiwemo ya Iringa, Mbeya, Moro, Pwani, Dar es Salaam, Tanga na Dodoma.

Alisema mradi wa IMAGE umekuwa ukitoa ufadhili wa Sh 800,000 kwa kila mwanafunzi kwa kila mwaka hatua ambayo imewezesha kutokatiza masomo yao na kufanya vizuri kitaaluma.

Aliwapongeza wanafunzi wanaomaliza akisema wamekuwa wakifanya vizuri katika mitihani yao yote ya ngazi ya shule, wilaya, mkoa na hata Taifa na katika mtihani wa Moko wa hivikaribuni shule hiyo ilikuwa ya tano kati ya shule 42 za wilaya hiyo.

Pamoja na mafanikio hayo, mkuu wa shule hiyo alitaja baadhi ya changamoto zinazoikabili shule hiyo kuwa ni pamoja na uchache wa vyumba vya madarasa, maabara na mabweni, vifaa vya maabara na vya kufundishia na ukosefu gari la shule; changamoto ambazo Mkuu wa Wilaya ya Kilolo aliahidi kushirikiana na uongozi wa shule hiyo kuzitafutia ufumbuzi.

Akiwashukuru IMAGE kwa ufadhili huo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza aliwapongeza wahitimu hao kwa kufanikiwa kuruka mitihani mingi ya kimaisha aliyosema ingeweza kukwamisha kiu yao ya kupata elimu hiyo.

“Msimamo wa serikali ni kuona mtoto wa kike anapata fursa ya elimu sawasawa na mtoto wa kiume kwa kuwa inatambua uwepo na uwezo wake na ndio maana ndani ya serikali wapo wanawake wanaoongoza sambamba na wanaume,” alisema.


Aliuomba uongozi wa shule hiyo kuangalia uwezekano wa kuanzisha kidato cha tano na sita katika shule hiyo ili kuwawezesha wanafunzi wanaokosa nafasi katika shule za serikali kuendelea na masomo hayo shuleni hapo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment