Monday, 9 October 2017

TAARIFA ZA MANGE KIMAMBI ZAFANYIWA KAZI, IGP AKATAA KUZUNGUMZA KINACHOENDELEA

MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro amesema jeshi hilo linaendelea na upelelezi wa taarifa za kuwakejeli na kuwatukana viongozi wa nchi zinazotolewa na mwanaharakati wa mitandao ya kijamii anayeishi Marekani, Mange Kimambi, lakini haliwezi kuziweka taarifa za upelelezi huo hadharani.

“Kwenye kazi hii ya upelelezi huwezi kuweka kila kitu wazi, tunajua (Mange) anavunja sheria za nchi; tunafanya nini, siwezi kusema,” alisema alipokuwa akizungumza na wanahabari katika viunga vya ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, mjini Iringa.

IGP Sirro alikuwa mjini Iringa leo katika ziara yake ya siku moja aliyotumia kufanya ukaguzi wa jeshi hilo, kuzungumza na maafisa wa polisi, askari polisi na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa.

Ametoa msimamo huo baada ya hivikaribuni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz kunukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema hawatamvumilia vitendo vinavyofanywa na Kimambi pamoja na kundi lake.

Katika taarifa hiyo, Boaz alisema jeshi hilo litawasaka na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola watu wanaoshirikiana na mwanaharakati huyo kutoa taarifa za uongo, uzushi, matusi na kejeli kwa viongozi wa nchi.

Pamoja na taarifa hiyo ya Kimambi, IGP Sirro alisema jeshi hilo litaendelea na jukumu lake la kulinda usalama wa raia na mali zao ikiwa ni pamoja na kuwasaka na kuwafikisha katika vyombo vya sheria waharifu wote wakiwemo wale wasiojulikana.

Akifafanua kuhusu waharifu wasiojulikana alisema; “kumekuwepo na changamoto ya matumizi ya neno hili. Kimsingi watanzania wanatakiwa kujua mtu anafanya tukio hakiwa hajulikani, na anapopanga kufanya uharifu huo haji Polii kutoa taarifa kwamba anataka kufanya uharifu.”

Akitoa mfano wa watu wasiojulikana alikumbusha kundi la waharifu waliokuwa wakifanya mauaji wilayani Kibiti ambao walijulikana baada ya kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya dola.

Katika nasaha zake kwa askari Polisi, alisisitiza wafanye kazi kwa kuzingatia maadili na haki ili wananchi walio katika maeneo yao waendelee kuishi kwa amani na utulivu, na waendelee kuliamini jeshi hilo.

Aliwataka wananchi wanaohitaji msaada wa askari na kuukosa kwasababu ya makosa yanayofanywa na askari hao watoe taarifa hizo kwa viongozi wa juu wa jeshi hilo au wengine wa serikalini ili wanaohusika waweze kuchukuliwa hatua.

“Hakuna askari polisi aliyepo juu ya sheria, akitenda kosa tuna taratibu zetu za kumshughulikia, anafukuzwa kazi na kupelekwa mahakamani,” alisema.

Alisema jeshi hilo pia lina kazi kubwa ya kutoa elimu kwa wananchi ili waachane na uharifu ukiwemo ule unaosababishwa na imani za kishirikiana.


“Kuna tatizo la ubakaji kwa watoto wa umri wa mdogo katika maeneo mbalimbali nchini kwasababu ya imani za kishirikina. Tuna kazi kubwa ya kutoa elimu kwa ndugu zetu wanaofanya uharifu huo, huwezi kupata utajiri kwa kubaka watoto,” alisema huku akiomba viongozi wa dini wasaidie kutoa elimu hiyo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment