Wednesday, 11 October 2017

MUFINDI VIJANA SACCOS YAWAKOPESHA BAJAJI MADEREVA WA BAJAJIMUFINDI Vijana Saccos ya wilayani Mufindi mkoani Iringa imetoa mkopo wa pikipiki za matairi matatu (Bajaji) 10 zenye thamani ya Sh Milioni 82.5 kwa wanachama wake vijana 10 jana, ikiwa ni miezi tisa tu toka ifufuliwe.

Saccos hiyo iliyoanzishwa mwaka 2013, ilikufa muda mfupi baadaye ikiwa na wanachama 136 kwasababu ya migogoro ya kiungozi kabla hajafufuliwa na kuanza kufanya kazi tena Januari, mwaka huu ikiwa na wanachama 60.

Mwenyekiti wa Saccos hiyo, Josephat Mkini alisema mikopo ya Bajaj hizo imetolewa na Saccos yao kwa kupitia Kampuni ya Sunbeam Auto Ltd ambao ni wasambazaji wakubwa wa Bajaji hizo nchini.

“Tangu tuanze kusambaza Bajaji hizi hapa nchini, hatujawahi kutoa mkopo wa aina hii popote pale zaidi ya Mufindi wanaokuwa wa kwanza kunufaika,” alisema mwakilishi wa kampuni hiyo Constantine Mayala.

Mayala alisema vijana waliopata mkopo huo wamebeba dhamana kubwa ya Saccos na wanachama wao, hivyo wanatakiwa kufanya marejesho yao kwa wakati ili mikopo hiyo iendelee kutiririka.

Akionesha imani yake kwa wanufaika wa mkopo huo, mwenyekiti wa Saccos hiyo alisema matarajio yao ni kutoa mikopo yenye thamani ya Sh Milioni 300 katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2017/2018.

“Tumeanza na mkopo wa bajaji 10, na kuanzia sasa kila baada ya miezi mitano  tutakuwa tukitoa mkopo wa bajaji zingine tano sambamba na mikopo ya fedha taslimu kuwezesha shughuli zingine za maendeleo za wanachama wetu,” alisema.

Akizungumzia marejesho ya mkopo wa Bajaji, Mkini alisema itakuwa Sh 25,000 kwa kila mkopaji kila siku na katika kipindi cha miezi 13 ijayo kila mmoja wao atakuwa amemaliza mkopo wake kama makubaliano yanavyotaka.

“Kabla ya mkopo huu wote tulikuwa madereva wa Bajaji za watu wengine; kila siku tulikuwa tunalipa Sh 20,000 kwa wenye bajaji hizo, sasa tuna fursa pana, tunachopata ni chetu, kwahiyo ni rahisi kufanya marejesho na kubakiwa na faida” alisema  Ungamo Nyamoga, mmoja wa wanufaika wa mkopo huo.

Mnufaika mwingine, Devota Mponzi alisema ana shauku kubwa ya kuona bajaji aliyokopeshwa inakuwa mali yake katika kipindi kifupi kijacho kwahiyo atatumia pia vyanzo vyake vingine vya mapato kukamilisha mkopo huo kabla ya wakati.

Afisa Biashara wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Evans Mtikile aliwapongeza vijana hao akisema halmashauri hiyo inaendelea na mpango wa kuboresha maegesho yaliyopo na kuanzisha mengine mapya ili kupanua wigo wa biashara hiyo.

Akikabidhi mikopo hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Jamuhuri William alisisitiza uaminifu akiwataka vijana hao wawe na nidhamu ya matumizi ya fedha ili wamudu kulipa madeni yao kwa wakati na kuifanya Saccos hiyo ipate mafanikio zaidi.

“Saccos nyingi zimeingia katika migogoro mikubwa na hata kufa kwasababu wanaokopa hawataki kufanya marejesho. Hatutegemei hili litokee kwenye Saccos hii, fanyeni vizuri ili mkopesheke zaidi,” alisema.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mafinga Mji Charles Makoga na wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Festo Mgina waliahidi kufanya kazi kwa ujirani na Saccos hiyo waliyosema ni ya mfano wilayani humo kwa kuwa na mafanikio kwa muda mfupi baada ya kutoka kwenye misukosuko.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment