Friday, 27 October 2017

MAWAKALA WA PEMBEJEO ZA RUZUKU KUPANDISHWA KIZIMBANI


ASILIMIA 100 ya mawakala wa pembejeo wanaoidai serikali wametakiwa kujiandaa kufikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa wakituhumiwa kutaka kuiibia serikali kwa kufanya udanganyifu kwenye hati zao za madai.

Akizungumza na baadhi ya mawakala hao mjini Iringa juzi, Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba alisema; “Itakuja orodha ya kila wakala na kiasi cha udanganyifu alichofanya. Asilimia mia moja ya mawakala walitaka kuipiga serikali, hii ni hatari kwa maendeleo ya Taifa.”

Ametoa taarifa hiyo ikiwa ni miezi miwili tangu Rais Dk John Magufuli atoe agizo kwa viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutokuwa na kigugumizi cha kuchukua hatua pale wanapokuwa na ushahidi wa watu wanaojihusisha na rushwa.

Akizungumza na wafanyakazi wa Takukuru katika ofisi za Makao Makuu ya taasisi hiyo jijini Dar es Salaam, Dk Magufuli alisema kuna mambo ya ovyo yanafanyika nchini na akatoa mfano wa uhakiki wa pembejeo za ruzuku uliobaini kuwepo kwa madai hewa ya Sh Bilioni 48.

“Tanzania ya ujanja ujanja imekwisha, mawakala kaeni tayari kwenda mahakamani. Wote mtakamatwa na kufunguliwa mashitaka kwa kutaka kuiba fedha za walipa kodi,” Dk Tizeba alisema huku baadhi ya mawakala hao wakinong’ona kuashiria kupinga.

Akifafanua jinsi mawakala hao walivyotaka kuiibia serikali, waziri huyo alitoa mfano akisema; “Tumebaini wengi wao wameongeza madai ya kile wanachostahili kulipwa. Kwa mfano wapo wanaodai Sh Milioni 30 lakini nyaraka zao zinaonesha wanatudai Sh Milioni 60.”

Akiwatahadharisha mawakala waliokuwa wanataka kupinga taarifa hiyo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza na wakuu wa wilaya zake zote, alisema serikali imejiridhisha pasipo shaka yoyote kwamba udanganyifu ulikuwa mkubwa na unachukiza.

“Na napenda niwajulishe kwamba wale wa wizarani kwangu ambao kwa namna moja au nyingine wameonekana kuhusika na madudu haya walikwishasimamishwa kazi na wakati wowote watafikishwa mahakamani kujibu mashtaka yao,” alisema.

Wakati huo huo, Dk Tizeba ametoa onyo kwa wafanyabiashara wa pembejeo za kilimo kuzingatia bei elekezi wakati wakisambaza pembejeo hizo kwa wakulima kwani serikali imedhamiri kwa dhati kupambana na bei holela zinazomnyonya mkulima.

“Hatua kali zitachukuliwa kwa wale wote watakaokiuka agizo hili la serikali lakini pia tutawashughulikia kwa mujibu wa sheria mawakala na wafanyabiashara watakaobainika kusambaza mbolea, mbegu na dawa feki kwa wakulima,” alisema.

Alitoa onyo kwa maafisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) na wa Mamlaka ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) kwamba watakuwa wa kwanza kuwajibishwa endapo itabainika katika msimu huu wa kilimo na mingine yote inayokuja kutakuwa na bidhaa hizo feki.

Alisema kwa miaka 56 ya Uhuru sekta ya kilimo imeshindwa kupiga hatua inayostahili kwasababu ya kulea changamoto zake mbalimbali zikiwemo za usambazaji wa pembejeo feki.

“Wapo wakulima wanauziwa mbegu hazioti, wapo wanauziwa majivu na mawe yaliyosagwa wakiamini ni mbolea na wapo wanaouziwa kile kinachoonekana ni dawa wakati si dawa. Haya yote yanafanyika na kumtia hasara mkulima na Taifa na hakuna hatua zinazochukuliwa,” alisema.

Alisema zile zama za wafanyabishara wa bidhaa za kilimo kutengeneza faida kwa kuwaibia wakulima zimefika mwisho huku serikali ya awamu ya tano ikidhamiria kwa dhati kubadili sura ya sekta hiyo ili iwe na tija zaidi.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment