Monday, 23 October 2017

MAKONDA AZUNGUMZIA BOMOABOMOA ILIYOTANGAZWA NA LUKUVIMkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewatoa hofu wakazi wake, akisema hakutakuwa na ubomoaji wa nyumba zao kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari leo.

Makonda ametoa tamko hilo baada ya vyombo vya habari leo Oktoba 23, 2017 kukariri taarifa ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa nyumba zote zilizojengwa bila ya vibali na ambazo zimejengwa katika viwanja vya dhuluma, zibomolewe.

Taarifa hiyo ilimkariri Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akiwaagiza wakurugenzi wa halmashauri, maofisa ardhi, ujenzi na mipango miji kuweka alama za "X" na kuvunja majengo yote yanayojengwa katika miji yao bila vibali na yale yanayojengwa katika viwanja vya watu wengine.

Hata hivyo, Waziri Lukuvi leo Jumatatu Oktoba 23,2017 ametoa ufafanuzi akisema kwa wale waliojenga kwenye viwanja vyenye hati za watu wengine kwa nguvu na kuwadhulumu wenye hati miliki haki yao ya kisheria, hatua zitachukuliwa ili kuwarudishia haki wanaostahili.

 “Hatutabomoa nyumba ya mtu bali tutaendelea na urasimishaji wa makazi kwa maeneo yaliyojengwa holela ili yawe makazi rasmi na wananchi wapelekewe huduma muhimu kama vile barabara, umeme na maji,” amesema Lukuvi.

“Muhimu wapewe hati miliki ili ziwasaidie kiuchumi na waweze kulipa kodi ya ardhi... lakini tutazuia ujenzi mpya holela katika miji yetu kwa mujibu wa sheria.”

Lukuvi, ambaye pia alipewa nafasi katika hafla ya kutunuku vyeti wajumbe wa kamati za makinikia na kufafanua ubomoaji huo, amesema viongozi wote wa wilaya na mitaa wahamasishe wananchi kushiriki kikamilifu katika urasimishaji wa makazi yao kwa faida yao na Taifa kwa jumla.

Kuhusu hilo, Makonda katika taarifa aliyoituma kwenye mitandao ya jamii, amesema Serikali inarasimisha makazi, akiwataka wananchi wenye mpango wa kujenga kufuata maelekezo ya Wizara ya Ardhi ili kuepuka kubomolewa.

Amesema kama ilivyofanyika Kimara ambako hati 6,000 zilitolewa kwa wananchi waliokuwa wamejenga kwenye makazi yasiyo rasmi, ndivyo itafanyika Oktoba 27,2017 kwa waliojenga Makongo Juu.

Makonda amesema kuna changamoto ya upatikanaji wa vibali vya ujenzi jambo alilosema halipaswi kuwa adhabu kwa wananchi waliojenga miaka ya nyuma.

Amesema changamoto hiyo ilisababisha mtu aliyekamilisha michoro kwa mujibu wa sheria na ana fedha za kuanza ujenzi kulazimika kufuatilia manispaa kwa miaka miwili hadi mitatu bila kupata kibali.


“Hata akipata watakuja watu wa OSHA (Mamlaka ya Usalama na Afya Kazini) kumsimamisha kwa madai hawana taarifa ya ujenzi jambo linalotengeneza mianya ya rushwa. Akimalizana na watu wa OSHA wanakuja watu wa kikosi cha zimamoto nao inabidi atafute utaratibu wa kumalizana nao, jambo linalokera wananchi na kuwafanya wakose hamasa ya kutafuta vibali vya ujenzi na hatimaye kujenga holela,” amesema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment