Saturday, 7 October 2017

MAGUFULI AWATEMA MAWAZIRI WANNE MABADILIKO YA BARAZA LA MAWAZIRI

Image result for baraza la mawaziri

Rais, Dkt. John Pombe Magufuli leo amefanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri ikiwa ni mara ya kwanza kufanya hivyo tangu aingie madarakani, ambapo mawaziri wanne waliokuwepo katika baraza la awali wamepigwa chini.

Katika mabadiliko hayo, Rais Magufuli ameongeza wizara mbili kutoka 19 hadi 21 na kuongeza Mawaziri wawili na manaibu watano.

Akitangaza mabadiliko hayo, Rais Magufuli amesema Wizara ya Nishati na Madini imegawanywa mara mbili, sasa kutakuwa na Wizara ya Nishati na Wizara ya Madini.

Amesema hatua hiyo inatokana na umuhimu wa rasilimali hiyo kwa taifa na kwamba wizara hizo zote kila moja itakuwa na waziri na naibu wake.

Rais Magufuli ametaja mabadiliko mengine katika Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambayo kwa sasa kutakuwa na Wizara ya Kilimo inayojitegemea na nyingine itakuwa ni Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Amesema sababu za kufanya mabadiliko hayo ni kutokana na umuhimu wa sekta hiyo inayoajiri asilimia 75 ya Watanzania nchini hivyo ni vyema ijitegemee.

Kila wizara itakuwa na waziri na naibu wake. Mabadiliko mengine ni katika wizara ya Tamisemi kwa kuweka nafasi mbili za manaibu waziri kwa sababu ni wizara inayogusa sehemu kubwa ya wananchi.

Mawaziri walioachwa ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe na nafasi yake imechukuliwa na Mhe. Hamis Kigwangwala aliyekuwa Naibu Waziri Wizara ya Afya.

Mwingine aliyeachwa ni aliyekuwa Waziri Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge ambaye nafasi yake imechukuliwa na Mbunge wa Katavi, Mhandisi Issack Kamwele aliyekuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni, Sanaa na Michezo, Annastazia Wambura naye amepigwa chini na nafasi yake imechukuliwa na Mbunge wa Viti Maalum CCM, Juliana Shonza.

Waziri wa Mazingira amebaki kuwa Mhe. January Makamba na Naibu wake atakuwa Mhe. Kangi Lugola. Aidha, aliyekuwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani naye ametupwa nje na nafasi yake imechukuliwa na Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga.

Rais Magufuli pia amemteua Angela Kairuki kuwa Waziri wa Madini na Naibu wake akiwa Haroun Nyongo huku akimteua Steven Kagaigai kuwa Katibu wa Bunge na aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo, Thomas Kashililah atapangiwa kazi nyingine.

Rais Magufuli amewashukuru watanzania kwa kuendelea kuwaunga mkono na kuwapongeza walioteuliwa.

Baraza Kamili la Mawaziri
Wizara ya Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika

Wizara ya Ofisi ya Rais Tamisemi Mawaziri – Suleiman Jafo, manaibu waziri – Josephat Kandege na Joseph George Kakunda.

Wizara ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Waziri – January Makamba, Naibu Waziri, Kangi Lugola.

Ofisi ya Waziri Mkuu: Sera, Bunge, Kazi Vijana, Ajira na Walemavu Waziri – Jenista Mhagama, manaibu Stella Ikupa na Anthony Mavunde.

Wizara ya Kilimo ni Dk Charles Tzeba na naibu wake Dk Mary Mwanjelwa.

Wizara wa Mifugo na Uvuvi ni Luhaga Mpina na naibu wake ni Abdallah Ulega Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa na manaibu wake Atashasta Nditiye na Elias Kwandikwa.

Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango na naibu waziri ni Ashantu Kijaji.

Wizara ya Nishati ni Dk Medard Kalemani na naibu wake ni Subira Mgalu.

Wizara wa Madini ni Angellah Kairuki na naibu wake Haruni Nyongo.

Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi Wizara wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk Augustino Mahiga na naibu Dk Susan Kolimba.

Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi Wizara ya Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba na naibu wake Hamad Masauni

Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na naibu ni Angelina Mabula.

Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangala na naibu wake ni Ngailonga Hasonga.

Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage na naibu wake ni Stella Manyanya.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako na naibu wake ni Wiliam Ole Nasha.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na naibu wake ni Dk Faustine Ndugulile.


Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe na naibu wake ni Juliana Shonza. Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Isack Kamwele na naibu wake ni Juma Aweso.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment