Monday, 30 October 2017

MAGOLI 13 YAPICHIKWA JUMAMOSI NA JUMAPILI LIGI YA SPANEST OKOA TEMBO
JUMLA ya magoli 13 yamefungwa Jumamosi na Jumapili katika kinyang’anyiro cha ligi ya kombe la SPANEST Piga Vita Ujangili, Okoa Tembo inayoendelea katika viwanja mbalimbali vya Tarafa ya Idodi na Pawaga.

Vijiji 24 vya tarafa hizo vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha vinashiriki ligi hiyo inayowaunganisha vijana na wadau wengine kushiriki vita dhidi ya ujangili.

Katika nyasi za viwanja vya Tarafa ya Pawaga zilizowaka moto Jumamosi ya Oktoba 28, Magozi FC na Mkombilenga FC walitoka sare ya bila kufungana huku Luganga ikipoteza pointi tatu muhimu katika uwanja wake wa nyumbani baada ya IloloMpya FC kuitandika 2-1.

Wakati bao la Luganga lilifungwa na Humphrey Luhunga yale ya Ilolompya yalifungwa na Hitson Mwashambwa na Mwinyi Kayugwa.

Mechi ingine ilikuwa kati ya Kisinga na Kinyika iliyomalizika kwa Kisinga kupoteza mchezo huo kwa mabao 3-1. Wakati bao la Kisinga lilifungwa na Selemeni Matibwa, magoli ya Kinyika yalifungwa na Amidy Mkosa na Selemani Mbwawa.

Nayo Isele FC ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya  Magombwe FC, bao lililofungwa na Joseph Chavalla huku Mkumbwanyi na Mboliboli wakitoka suluhu ya 0-0.

Katika mechi za Jumapili zilizopogwa katika viwanja vya tarafa ya Idodi, Malizanga FC na Mafuruto FC walitoka 1-1 mabao yaliyofungwa na Said Mtuga na William Sama.

Mapogolo FC na Tungamalenga FC walitoka 0-2 mabao yote mawili ya Tungamalenga yakifungwa na Emanuel Sade huku Makifu FC akipoteza mchezo katika uwanja wake wa nyumbani kwa kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Mahuninga FC, bao lililofungwa na Lemmy Ngetwa.

Ligi hiyo iliyoanza Octoba 21, itaendelea tena wiki hii katika viwanja mbalimbali vya vijiji vya tarafa hizo, wilaya ya Iringa.

Mshindi wa kwanza wa ligi hiyo itakayopigwa kwa mwezi mmoja ataondoka na kombe, medali za dhahabu, seti moja ya jezi, cheti, Sh Milioni Moja taslimu na atapata fursa ya kutembelea hifadhi ya taifa ya Ruaha.

Na mshindi wa pili ataondoka na medali za shaba, cheti, mipira miwili na Sh 700,000 taslimu, huku mshindi wa tatu akioondoka na cheti, medali na Sh 500,000.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment