Thursday, 26 October 2017

MABINGWA WATETEZI SPANEST CUP WALAZIMISHWA SARE
Kitisi FC wamelazimishwa sare ya 1-1 na Tungamalenga FC katika harakati zao za kutetea Kombe la SPANEST Piga Vita Ujangili Okoa Tembo, mchezo uliopigwa jana katika ligi ya kombe hilo inayoshirikisha timu 24 za vijiji vya Tarafa ya Idodi na Pawaga vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Katika mchezo wao wa kwanza Kitisi FC iliifunga Mapogoro FC kwa mabao 2-1 na hivyo kufufua matumaini ya kutwaa kombe hilo kwa mara ya pili mfululizo mwaka huu.

Pamoja na kuambulia pointi moja katika mchezo huo uliochezwa katika uwanja wake wa nyumbani, wachezaji wa Kitisi FC wamesema wako katika hali nzuri na wana imani watatea ubingwa huo.

Matokeo mengine katika mechi za juzi ni pamoja na Kinyika FC walioilaza Isele kwa 1-0 kwa bila kupitia mshambuliaji wake Goodluck Mgimwa, nao Mbuyuni FC walipoteza mechi yao ya nyumbani kwa kufungwa bao 1-0 na Kimande FC.

Ilolompya FC na Magozi walitoka sare ya bila kufungana kama ilivyokuwa kwa Magombwe FC na Kisinga FC huku Idodi FC ikiibamiza bila huruma Mapogoro FC kwa bao 1-0 na hivyo kuifanya timu hiyo ipoteze michezo miwili mfululizo.

Ligi hiyo iliyoanza Octoba 21, imeendelea tena leo katika viwanja mbalimbali vya vijiji hivyo.

Mshindi wa kwanza wa ligi hiyo itakayopigwa kwa mwezi mmoja ataondoka na kombe, medali za dhahabu, seti moja ya jezi, cheti, Sh Milioni Moja taslimu na atapata fursa ya kutembelea hifadhi ya taifa ya Ruaha.

Na mshindi wa pili ataondoka na medali za shaba, cheti, mipira miwili na Sh 700,000 taslimu, huku mshindi wa tatu akioondoka na cheti, medali na Sh 500,000.


SPANEST ilianzisha ligi hiyo ikilenga kuwaunganisha vijana wa vijiji hivyo na wadau wengine katika pembe zote za nchi kushiriki katika vita dhidi ya ujangili, hatua ambayo imeleta mafanikio makubwa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment