Monday, 9 October 2017

MAANDALIZI YA LIGI YA SPANEST, PIGA VITA UJANGILI OKOA TEMBO YAIVA


TIMU 24 za vijiji vya tarafa ya Idodi na Pawaga vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha zitashiriki Ligi ya Kombe la Spanest itakayoanza kutimua vumbi Oktoba 21, mwaka huu ikiwa imebeba kauli mbiu yake ya ‘Piga Vita Ujangili, Okoa Tembo”.

Ligi hiyo inayoratibiwa na Mradi wa Kuboresha Mtandano wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (Spanest) kwa usimamizi wa Chama cha Mpira wa Miguu Iringa Vijijini (IRFA) inafanyika katika tarafa hizo kwa mwaka wa nne sasa.

Akizungumza na wanahabari leo mjini Iringa, Mratibu wa Spanest Godwell Ole Meing’ataki alisema mshindi wa kwanza wa ligi hiyo itakayopigwa kwa mwezi mmoja ataondoka na kombe, medali za dhahabu, seti moja ya jezi, cheti, Sh Milioni Moja taslimu na atapata fursa ya kutembelea hifadhi ya taifa ya Ruaha.

Alisema wakati mshindi wa pili wa ligi hiyo ataondoka na medali za shaba, cheti, mipira miwili na Sh 700,000 taslimu, mshindi wa tatu ataondoka na cheti, medali na Sh 500,000.

"Zawadi na vifaa vyenye thamani ya takribani Sh Milioni 12 kwa ajili ya ligi hiyo vipo tayari. Tunasubiri kukamilisha taratibu chache zilizobaki ili ligi hiyo ianze kutimua vumbi," alisema.

Meingataki alisema wameanzisha ligi hiyo wakilenga kuwaunganisha vijana katika vita ya ujangili kutokana na ukweli kwamba vijana wengi wamekuwa wakishawishiwa kuingia kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na kufanya ujangili.

Akipokea kombe na vifaa vingine kwa ajili ya ligi hiyo, Katibu wa IRFA, Juma Lalika alisema ligi hiyo itakuwa ya mtoano na timu shiriki zitamenyana nyumbani na ugenini.

Alisema timu nane zitakazosalia katika mtoano huo, zitaingia robo fanaili; hatua itakayowezesha timu hizo kuingia nusu fainali, fainali na kutafuta mshindi wa tatu.

Katibu tarafa wa Idodi, Yacob Kiwanga na wa tarafa ya Pawaga, Alli Ngweja ambao tarafa zao zinaunda vijiji hivyo wamesema ligi hiyo imeleta hamasa kubwa kwa vijana na wananchi wao  vkuupenda mchezo huo unaotumika pia kutolea elimu ya uhifadhi, utalii na kuhamasisha shughuli zingine za maendeleo.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment