Tuesday, 24 October 2017

KITISI FC YAANZA VYEMA KUTETEA UBINGWA WA KOMBE LA SPANEST OKOA TEMBO
Mabingwa watetezi wa Kombe la SPANEST linalolenga kuwahamasisha wadau mbalimbali kupiga vita ujangili na kuokoa Tembo wa mwaka 2016, Kitisi FC wameanza vyema kampeni yao ya kulitetea kombe hilo mwaka huu kwa kuitwanga bila huruma Mapogolo FC kwa mabao 2-1.

Mchezo huo wa kusisimua ulipigwa Oktoba 22 katika uwanja wa nyumbani wa Mapogolo, ikiwa ni siku moja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza kuzindua ligi hiyo inayoshirikisha timu 24 za vijiji vya tarafa ya Idodi na Pawaga vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Katika uzinduzi wa ligi hiyo, Itunundu FC, mabingwa wa ligi hiyo wa mwaka 2014 walionesha umwamba wao kwa kuwachapa bila huruma wapinzani wao wa jadi Kimande FC kwa bao 1-0; mchezo uliopigwa katika uwanja wa Kimande Pawaga, Iringa Vijijini.  

Mabao mawili ya Kitisi FC yalifungwa na Maneno Charles na Lucas Kidunye katika mchezo uliopigwa katika uwanja wa nyumbani wa Mapogolo FC, Iringa Vijijini.

Mapogolo FC ilijituma na kupata bao moja la kufutia machozi kupitia kwa Enock Ngilando lakini bado ilionekana kushindwa kuhimili vishindo vya Kitisi FC katika mchezo huo wenye mashabiki wengi.

Timu nyingine zilizoshuka dimbani Oktoba 22, mwaka huu ni pamoja na Nyamahana na Malizanga waliotoka sare ya bila kufungana.

Nao Tungamalenga FC na Idodi FC waliotoka sare ya bao 1-1, magoli yaliyofungwa na Paulo Biria na Sharifu Gembe

Mechi nyingine iliwakutanisha Kisilwa FC 2 na Makifu FC 0, mabao yaliyofungwa na Patrick Kisakanyike na Thomas Kiyasile.

Ligi hiyo iliyopumzika Jumatatu itaendelea tena Jumanne na Jumatano katika viwanja mbalimbali vya soka Iringa Vijijini.

Wakati Mahuninga FC itaikaribisha katika uwanja wake wa nyumbani Kisilwa FC siku ya Jumanne, Mafuluto FC itakuwa mwenyeji wa Nyamahana FC.

Katika ligi hiyo yenye makundi yatakayotoa washindi nane watakaoingia hatua ya robo fainali, Ilolo FC itakuwa mwenyeji wa Magozi FC katika mchezo utakaopigwa Jumatano, . Mkombilenga FC itamenyana na Luganga FC, Kimande FC na Itunundu FC na Mboliboli FC itakuwa mwenyeji Mbugani FC..

Mratibu wa Spanest Godwell Ole Maing’ataki amesema mshindi wa kwanza wa ligi hiyo itakayopigwa kwa mwezi mmoja ataondoka na kombe, medali za dhahabu, seti moja ya jezi, cheti, Sh Milioni Moja taslimu na atapata fursa ya kutembelea hifadhi ya taifa ya Ruaha.

Amesema wakati mshindi wa pili wa ligi hiyo ataondoka na medali za shaba, cheti, mipira miwili na Sh 700,000 taslimu, mshindi wa tatu ataondoka na cheti, medali na Sh 500,000.


Meingataki amesema wameanzisha ligi hiyo wakilenga kuwaunganisha vijana katika vita ya ujangili kwa kuzingatia ukweli kwamba vijana wengi wamekuwa wakishawishiwa kuingia kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na kufanya ujangili.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment