Friday, 27 October 2017

KINYANG'ANYIRO KOMBE LA SPANEST CHAZIDI KUNOGA


MAMIA ya wapenzi wa soka jana walijitokeza kwa wingi katika uwanja wa Mafuruto kushuhudia vijana wao wa Mafuruto FC wakiweka kibindoni pointi tatu muhimu baada ya kuikanyaga bila huruma Nyamahana FC kwa mabao 2-1.

Mabao ya timu hizo mbili zinazowania Kombe la SPANEST Piga Vita Ujangili, Okoa Tembo linaloshirikisha timu 24 za vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha; yalitiwa wavuni kipindi cha pili cha mchezo huo baada ya nusu ya kwanza ya mchezo huo kumalizika kwa sare bila kufungana.

Wakati mabao ya Mafuruto FC yaliwekwa kimiani na Vicent Sanga na Batazaly Kiseo, Nyamahana FC walipata bao lao la kufutia machozi kupitia kwa mshambuliaji wake Maneno Chengula.

Katika mchezo mwingine uliochezwa jana kuwania kombe hilo linalohamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika vita dhidi ya ujangili, Mahuninga FC na Kisilwa FC walishindwa kuoneshana ubabe na kumaliza zote 90 za mchezo bila kufungana.

Ligi hiyo iliyoanza Octoba 21, inaendelea tena kesho Jumamosi katika viwanja mbalimbali vya vijiji hivyo vya wilaya ya Iringa.

Mshindi wa kwanza wa ligi hiyo itakayopigwa kwa mwezi mmoja ataondoka na kombe, medali za dhahabu, seti moja ya jezi, cheti, Sh Milioni Moja taslimu na atapata fursa ya kutembelea hifadhi ya taifa ya Ruaha.

Na mshindi wa pili ataondoka na medali za shaba, cheti, mipira miwili na Sh 700,000 taslimu, huku mshindi wa tatu akioondoka na cheti, medali na Sh 500,000.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment