Thursday, 26 October 2017

DK TIZEBA AIPIGA STOP KAMPUNI YA TUMBAKU KUNADI MALI ZAKE

Image result for Dk Tizeba

MAMLAKA za serikali zimeagizwa kuchukua hatua za haraka kuizuia kampuni ya ununuzi wa Tumbaku nchini, Tanzania Leaf Tobacco Company (TLTC) yenye makao makuu yake mjini Mrogoro kuendelea na azma yake ya kuuza mali zake zote mpaka pale zitakapofanyiwa uhakiki.

Agizo hilo limetolewa leo na Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba alipokuwa akizungumza na wasambazaji wa pembejeo za kilimo wa mkoani Iringa.

“Katika moja ya magazeti ya kila siku nchini, kampuni hiyo iliweka tangazo, ikitangaza kuuza mali zake zote jambo linaloashiria haitafanya tena kazi ya ununuzi wa tumbaku nchini,” alisema.

“Mali wanazotaka kuuza ni mali walizozikuta, waliuziwa na Bodi ya Tumbaku….nadhani mwaka 2009 na uuzwaji wenyewe hakuwa wazi sana,” alisema.

Alisema kampuni hiyo iliuziwa mali hizo zilizoko katika maeneo mbalimbali nchini ili isaidie kuendeleza ukuaji wa kilimo cha tumbaku nchini na biashara yake.

“Baada ya kuuziwa waliendelea kusindika tumbaku pale Morogoro na ni moja kati ya kampuni kubwa zilizokuwa zinanunua tumbaku inayozalishwa na wakulima katika maeneo mbalimbali nchini,” alisema.

Alisema serikali imeshtushwa kusikia kampuni hiyo inatangaza kuuza mali zake zote katika kipindi ambacho zaidi ya kilo milioni 21 za tumbaku zilizozalishwakwa nyakati tofauti nchini, hazina soko.

“Kwahiyo naelekeza mamlaka zote za serikali na vyombo vyake vyote wazuie kampuni hiyo kuuza mali ili serikali ijiridhishe kama wanachotaka kufanya ni sahihi na nia ya kufanya hivyo ni sahihi,” alisema.

Alimuagiza Mkurugenzi wa Bodi ya Tumbaku nchini kuiandika barua kampuni hiyo haraka iwzekanavyo kabla haijaanza kufanya mnada wa mali hizo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment