Monday, 25 September 2017

WAZIRI MKUU KUZINDUA MAONESHO YA KARIBU KUSINI SEPTEMBA 29 MJINI IRINGAMKUU wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza amewaomba wananchi wa manispaa ya Iringa kuunga na wageni kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kujitokeza kwa wingi kushuhudia maonesho ya utalii ya Karibu Kusini yatakayofanyika kwa mara ya pili mjini Iringa kati ya Septemba 27 na Oktoba 2, mwaka huu.

Akizungumza na wanahabari ofisini kwake hii leo, Masenza amesema Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Kasimu Majaliwa amealikwa kuyazindua maonesho hayo yaliyoandaliwa na mikoa ya nyanda za juu kusini kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii,  shirika la kuhudumia viwanda vidogo (Sido) na wadau mbalimbali ukiwemo Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST).

Amesema maonesho hayo yatazinduliwa Septemba 29, ikiwa ni siku mbili mbele baada ya kufunguliwa Septemba 27 na kwamba hadi leo wadau 362 wamethibitisha ushiriki wao wa maonesho hayo yanayokwenda sambamba na kauli mbiu ya ‘Utalii ni Nguzo ya Uchumi wa Viwanda’.

Amesema lengo kuu la maonesho hayo ni kutangaza fursa na vivutio vilivyoko katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ili wageni wa ndani na nje waweze kutembelea.

“Tuna vivutio vya kihistoria, kiutamaduni na kiikolojia vinavyofanya upekee wa mikoa hiyo katika utalii, “ amesema .

Alisema vivutio hivyo vikitembelewa vitaongeza ajira kwa wananchi, mapato na kupanua fursa za uwekezaji hivyo kuongeza umuhimu wa utunzaji wa mzuri wa maliasili na mazingira.


Kwa kupitia maonesho hayo, Masenza alisema  wajasiriamali watapata fursa ya kuonesha na kuuza bidhaa zao, na kutakuwepo na utoaji wa elimu katika sekta mbalimbali zinazogusa mambo ya utalii.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment