Thursday, 14 September 2017

WAKATAA KUACHA POMBE, WASEMA HIYO NI LISHE INAYOWAPA NGUVU


BAADHI ya wananchi wa kijiji cha Wangama wilayani Kilolo mkoani Iringa wamesema pombe ya kienyeji aina ya Komoni wanayoitengeneza kwa mahindi na ulezi ni chakula chao cha asili cha kila siku ambacho hawawezi kukiacha katika mazingira yoyote yale.

Waliyasema hayo hivikaribuni kwa mkuu wa wilaya hiyo, Asia Abdallah aliyetembelea kijiji hicho kujionea maendeleo yake ya elimu na kuwakuta baadhi yao wakinywa pombe hiyo muda wa kazi.

“Pombe ndio kila kitu kijijini hapa, hatuwezi kuacha, hicho ni chakula chetu cha asili. Ni lazima tunywe ndio tufanye kazi nyingine,” alisema mmoja wao aliyejitambulisha kwa jina Michael.

Wakizungumza na mkuu wa wilaya huyo, wananchi hao walisema wanajisikia fahari kutumia kinywaji hicho wakati wowote wanapotaka wakiamini ndicho kinachowaongezea nguvu mwilini na ni burudani inayowafanya wafurahie maisha ya kijijini.

 “Hapa kijijini hakuna mtu anayeweza kwenda shamba na kulima bila kunywa pombe na wengi wetu hatuwezi kula chakula mpaka tunywe. Ni asili yetu, ni utamaduni wetu. Tutakuwa waongo kama tutakudanganya mkuu wetu wa wilaya kwamba tunaweza kuacha,” alisema Rashid Ramadhani huku akishangiliwa na wananchi wengine.

Ramadhani alisema asilimia 95 ya wananchi wa kijiji hicho wanatumia kinywaji hicho kwa wastani wa lita kati ya nne na kumi kwa siku na imekuwa biashara yenye soko la uhakika kwa akina mama wengi kijijini hapo.

Akionekana kusikitishwa na hali hiyo, mkuu wa wilaya hiyo aliahidi kurudi kijijini hapo kwa mara nyingine tena ili apate kuzungumza na wananchi hao kwa kina kuhusu sheria na madhara ya matumizi ya pombe kupita kiasi.

“Nchi inaongozwa kwa sheria na ina taratibu zake. Hakuna mtu anayeruhusiwa kuendesha mambo kwa mazoea bila kufuata sheria,” alisema.

Alisema kwa kuzingatia sheria na taratibu hizo watu hawaruhusiwi kunywa pombe wakati wa kazi kwani kwa kufanya hivyo wanazorotesha maendeleo lakini pia ni hatari kwa afya zao.

“Nikiwaanngalia hapa naona kila mtu wakiwemo watoto wadogo wameshaelewa. Mnaweza kufikiri ni ufahari kunywa pombe kupita kiasi, wito wangu ni lazima mnywe kwa kiwango na kwa wakati,” alisema.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Ephraim Mbatule alisema unywaji wa pombe katika kijiji hicho chenye wakazi 590 ni mkubwa japokuwa hauthiri shughuli za maendeleo.


“Wananchi wanashiriki katika shughuli za ujenzi wa miradi mbalimbali ya kijiji kama ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu na zinginezo. Pamoja na ushiriki wao tutaendelea kutoa elimu ili wapunguze unywaji huo wa pombe kwa kuwa una madhara makubwa kiafya,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment