Saturday, 9 September 2017

UBALOZI WA JAPAN NA INDIA KUSAIDIA KUBORESHA SEKTA YA AFYA KILOLO


UBALOZI wa Japan na India nchini umeahidi kusaidia juhudi za serikali ya wilaya ya Kilolo mkoani Iringa kuboresha huduma za afya kwa ustawi wa wananchi wake kwa kutoa misaada mbalimbali ya vifaa tiba.

Wakati ubalozi wa Japan umeahidi kutoa gari la kubeba wagonjwa kwa halmashauri ya wilaya hiyo, ubalozi wa India kwa kupitia naibu balozi wake umeahidi kuyafanyia kazi maombi yake ya vifaa tiba.

Akizungumza na mtandao huu mjini Iringa, Abdalla alisema Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) nao wameahidi kutoa msaada wa baadhi ya vifaa tiba  kwa ajili ya hospitali ya wilaya hiyo inayotarajiwa kuanza kutoa huduma wakati wowote mwakani baada ya awamu ya kwanza ya ujenzi wake kukamilika.

“Balozi hizo na NSSF zilitoa ahadi hizo hivikaribuni baada ya mimi na maafisa wengine wa halmashauri ya wilaya ya Kilolo kuwasilisha maombi yetu kwao, jijini Dar es Salaam,” alisema.

Katika safari hiyo, mkuu wa wilaya huyo aliambatana na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Aloyce Kwezi, mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, Valance Kihwaga, mbunge wa jimbo hilo Venance Mwamotto na maafisa wengine wa wilaya hiyo.

Akizungumza maendeleo ya ujenzi wa hospitali hiyo hivikaribuni, Kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Dk John Mwingira alisema hadi kukamilika kwake awamu hiyo itatumia zaidi ya Sh Bilioni 4.2.

Alisema awamu hiyo iliyoanza kujengwa mwaka 2011 inahusisha ujenzi wa jengo la mionzi, jengo la kupokelea wagonjwa (OPD), jengo la utawala, jengo la huduma ya mama na mtoto, jengo la maabara na jengo la kulaza wagonjwa 56.

“Ujenzi wa jengo la upasuaji na chumba cha kuhifadhia maiti haujaanza lakini halmashauri imeshafanya makubaliano na SUMA JKT pindi fedha zitakapoletwa, ujenzi uanze mara moja,” alisema huku akisisitiza kwamba huduma hizo zitaanza kutolewa mwakani.

Alisema kwasasa wilaya ya Kilolo inaitumia hospitali ya Ilula inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa kama hospitali yake teule ya wilaya.

Kwa kuzingatia ramani ya wizara ya afya, wanawake, jinsia, wazee na watoto, Dk Mwingira alisema ili kukamilisha miundombinu yote ya hospitali hiyo zaidi ya Sh Bilioni 12 zinahitajika.

“Itakapokamilika hospitali hii inalenga kuhudumia zaidi ya wakazi 230,000 kutokana na kasi ya ongezeko la watu wilayani hapa linalokadiriwa kuwa asilimia 1.7 kwa mwaka,” alisema. 

Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Asia Abdallah alisema wilaya hiyo itaendelea kushirikisha wadau wake wa ndani na nje kuhakikisha miundombinu yote inayohitajika inakamilika.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza aliipongeza wilaya hiyo kwa hatua waliyofikia katika ujenzi huo akisema hospitali hiyo itaiwezesha kupunguza kiwango cha maambukizi ya VVU/Ukimwi, magonjwa na vifo vya watoto na akina mama wajawazito, kupunguza uhitaji wa rufaa za wagonjwa na kukabiliana na uhitaji mkubwa wa huduma za dharula.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment