Monday, 25 September 2017

MCHUNGAJI MSIGWA AMGEUZIA KIBAO OCD IRINGA

Image result for mchungaji peter msigwa

MBUNGE wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa ametangaza kumfunguli mashitaka ya matumizi mabaya ya madaraka mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Iringa (OCD).

“Mawakili wangu wanaendelea kulifanyia kazi shauri hilo na wakati wowote OCD huyo atashitakiwa yeye kama yeye kwa kosa hilo,” alisema wakati akizungumza na wanahabari hii leo.

Hatua hiyo imekuja saa kadhaa baada ya Jeshi la Polisi Wilayani Iringa jana majira ya saa 11.30 kumkamata, kumuhoji na baadaye kumuachia kwa dhamana kwa tuhuma ya kutoa maneno ya uchochezi yaliyokuwa yakilenga kuchonganisha vyombo vya dola na wananchi na kutia hofu jamii.

Mchungaji Msigwa amemtuhumu OCD huyo kuzuia mikutano yake na wapiga kura wake wa Jimbo la Iringa mjini aliyoanza kuifanya jana baada ya kutoka Nairobi nchini Kenya alikokuwa akisaidia kumuuguza Mbunge wa Singida Mashariki na Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu aliyenusurika kuuwa baada ya kushambuliwa kwa risasi nyingi na watu wasiojulikana.

“Mimi nimetuhumiwa kufanya uchochezi, anayeweza kunihukumu kwa kosa hilo ni mahakama tu, sasa kwanini mikutano yangu isitishwe kabla mahakama haijatoa maamuzi?” alisema.

Pamoja na kufungua mashitaka hayo, mbunge huyo amesema ataka rufaa kwa waziri mwenye dhamana na bunge kupinga uamuzi wa jeshi la Polisi kumfungulia kesi ya uchochezi wakati akitekeleza majukumu yake.

Akikana kufanya uchochezi kwa mujibu wa sheria ya uchochezi Mchungaji Msigwa alisema anao wajibu wa kuwachochea wananchi wawe na macho mengi ya kuona makosa ya serikali iliyopo madarakani ili wasiichague katika chaguzi zijazo.

“Kitendo cha Jeshi la Polisi kunikamata wakati nikihutubia wananchi wangu, ni udhalilishaji wa Bunge kama taasisi lakini pia wamenidhalilisha mimi mwenyewe kwasababu katika mkutano ule sikuwa nafanya jambo lolote la kihalifu,” alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Julius Mjengi alithibitisha kukamatwa kwa mbunge huyo huku akisema watamfikisha mahakamani wakato wowote kuanzia sasa baada ya uchunguzi wa tukio hilo kukamilika.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment