Sunday, 24 September 2017

MAREKANI YAANZA KUMSOGELEA KOREA KASKAZINI KIJESHI

Korea-Conflict 2017, US B-1 B-Bomber

Wakati viongozi wa mataifa ya Marekani na Korea Kaskazini wakiendelea kutunishiana misuli, ndege za Kijeshi za Marekani zimepaa karibu na pwani ya mashariki ya Korea Kaskazini katika kuonyesha ubabe wa kivita, idara ya ulinzi nchini Marekani Pentagon imesema.

Msemaji wa Idara hiyo, Dana White amesema kuwa hatua hiyo ni kuonyesha kuwa Rais Trump ana njia tofauti za kijeshi kushinda vitisho vyovyote vile.

Marekani na Korea Kaskazini zimerushiana maneno makali katika kipindi cha siku chache zilizopita ambapo akihutubia Umoja wa Mataifa, Rais Trump alitishia kulifutilia mbali taifa la Korea Kaskazini huku kiongozi wa Pyongyang, Kim Jong-Un akihutubia maelfu ya wananchi wake amesema kuwa Rais Trump atakula maneno yake mwenyewe.

Katika Umoja wa Mataifa siku ya Jumanne, Rais Trump alisema kuwa ataiangamiza Korea Kaskazini iwapo Marekani italazimika kujitetea na washirika wake.

“Hili ni eneo ambalo jeshi lolote halifai kupitia na ni ndege za kijeshi za Marekani ambazo zimeweza kulifikia katika karne ya 21, licha ya tabia mbaya ya Korea Kaskazini,” amsema Bi White.

Tangazo hili lilijiri muda mfupi kabla ya Waziri wa Kigeni wa Korea Kaskazini kutoa hotuba yake katika umoja wa mataifa .


Mapema siku ya Jumamosi, tetemeko lenye ukubwa wa 3.4 katika vipimo vya Ritcher lilisikika karibu na kituo cha kujaribia makombora cha Korea Kaskazini na kuzua hofu kwamba taifa hilo huenda lilitekeleza jaribio jingine la kombora lake lakini wataalam wamesema kuwa lilikuwa tetemeko la ardhi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment