Thursday, 7 September 2017

MAFINGA YAANZA MCHAKATO WA UJENZI WA MJI WA KISASA


MKUU wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza amezindua mchakato utakaokuja na Mpango Kabambe (Master Plan) wa Mji wa Mafinga huku akitaka kukamilika kwa fursa hiyo kuende sambamba na kuufanya mji huo kuwa wa viwanda vikubwa vya bidhaa za mbao.

Mafinga ni moja kati ya halmashauri mbili zinazounda wilaya ya Mufindi ambayo ni kinara nchini kwa uzalishaji wa aina mbalimbali za miti ya kupandwa.

Akiwahutubia wadau mbalimbali waliojitokeza katika uzinduzi huo, Masenza alimwagiza mkurugenzi wa halmashauri ya mji huo kusimamamisha taratibu za kuendeleza mji huo ili kusubiri Mpango Kambambe huo.

Kuhusu taratibu ndani ya eneo la Mpango Kabambe, mkuu wa mkoa amewataka wananchi waondolewe hofu ya kupoteza ardhi zao kwani mpango hauji kunyang’anya ardhi bali kuongeza thamani.

“Kwa wale watakao lazimika kupisha maeneo kwa ajili ya kuruhusu aina ya ujenzi uliopendekezwa katika mpango, watalipwa fidia katika thamani ya ardhi yao. Aidha mamlaka ya kiutawala pia haitabadilika,” alisema Masenza.

Awali mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Saada Mwaruka alisema sehemu kubwa ya mji wa Mafinga wenye kilometa za mraba 953 umeendelezwa kiholela jambo ambalo ni kero kubwa katika ukuaji wa mji huo.

Kuhusu faida za Mpango Kabambe, Mwaruka alisema utasaidia kukabiliana na ongezeko la watu,  utaharakisha upangaji na upimaji wa rdhi, utapunguza migogoro ya ardhi, utawezesha upatikanaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi na hatimaye utachochea watu kwenda kuwekeza na hatimaye utaifikisha Mafinga katika uchumi wa viwanda.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jamuhuri William amemshukuru mkuu wa mkoa kwa kuzindua mchakato huo akisema Mafinga yenye sura nzuri kwa miaka mingi ijayo inakuja.

Afisa Ardhi na Mipango Miji wa halmashauri hiyo, Rajabu Gogwa alisema ongezeko la makazi, viwanda na ongezeko la watu ni moja ya mambo yaliyowasukuma kuanzisha mchakato wa kupata mpango huo.

Kwa kupitia mpango huo, Gogwa alisema kutakuwa na maeneo yatakayotengwa kwa ajili ya shughuli za biashara, huduma za fedha, makao makuu ya taasisi mbalimbali, hoteli na majengo marefu na ya kisasa.

Aidha kutakuwa na maeneo ya viwanda vikubwa, vya kati na vidogo, maeneo ya elimu, makazi yatakayopangwa na kuratibuwa kwa ustadi wa hali ya juu, maeneo ya huduma za afya, michezo, huduma za usafiri, maeneo ya wazi na ya shughuli za kilimo.

Awali mwakilishi kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi, Profesa Aldo Lupala alisema ni muhimu watanzania wakazingatia kwamba ukuaji wa miji wenye tija ni ule unaoenda sambamba na mapinduzi ya viwanda.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment