Monday, 25 September 2017

DC KILOLO AAGIZA WANAOLIMA KWENYE VYANZO VYA MAJI WAONDOKE


MKUU wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdallah amewataka wananchi wanaolima vinyungu kwenye maeneo oevu wilayani humo kujiandaa kisaikolojia kuondoka katika maeneo hayo ili kutii amri ya serikali ya kulinda vyanzo vya maji.

Aliyasema hayo hivikaribuni kijijini Udekwa wilayani humo wakati akizindua mchakato wa kupata washindi wa tuzo ya hifadhi ya mazingira kwa mwaka 2017/2018 inayotolewa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa mwaka wa tatu sasa.

Mbali na Kilolo, wilaya zingine zinazoshiriki shindano la tuzo hizo ni Mufindi, Makete, Wanging’ombe na Mbarali ambazo kwa pamoja zina vyanzo vingi vya maji yanayotiririka kuelekea Mto Ruaha Mkuu.

Mhifadhi Mwandamizi wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambako mto huo unapita na ndio chanzo kikuu cha maji kwa wanyama wa hifadhi hiyo, Moronda Moronda alisema tuzo hiyo ambayo mshindi wake wa kwanza anapata Sh Milioni 2, wa pili Sh Milioni 1.5 na wa tatu Sh Milioni 1 imeganyika katika makundi matano.

Aliyataja makundi hayo kuwa ni uhamasishaji na uelimishaji uhifadhi wa mazingira, uhifadhi wa vyanzo vya maji na kingo za mito, upandaji na utunzaji wa miti ya asili, uhifadhi wa ardhi na uhifadhi wa mapito (shoroba) ya wanyama.

Meneja wa Ujirani Mwema wa Tanapa, Ahamed Mbugi alisema tuzo hiyo inatolewa kwa majaribio ya miaka mitatu katika wilaya hizo na kwamba itapelekwa katika wilaya zingine zinazopakana na hifadhi za Taifa mbalimbali nchini kutokana na mafanikio yake.

Akisisitiza umuhimu wa wananchi wanaolima katika vyanzo vya maji kuondoka katika maeneo hayo kabla mkono wa sheria haujawafikia, Mkuu wa wilaya ya Kilolo alisema; “Mnatakiwa kutii sheria bila shuruti, ondokeni katika maeneo hayo, tafute maeneo mengine kwani wilaya hii ina maeneo mengine mengi yanayofaa kwa kilimo.”

Akizungumzia umuhimu wa bonde la mto Ruaha Mkuu kwa maendeleo ya nchi, DC Abdallah alisema mbali na hifadhi ya Taifa ya Ruaha kuwa katika bonde hilo, shughuli mbalimbali za uchumi ikiwemo ya uzalishaji wa umeme katika bwawa la Mtera inategemea bonde hilo.

“Lakini pia bonde hilo ndilo linalomwaga maji katika bonde la Kilombero na Rufiji ambayo hutegemewa na mamilioni ya watanzania kwa shughuli za uzalishaji mali kikiwemo kili, ufugaji na uvuvi,” alisema.

Pamoja na umuhimu wote huo alisema bonde hilo linakabiliwa na uharibifu mkubwa wa mazingira hususani uharibifu wa mazingira ya ardhi na vyanzo vya maji.

Akipokea agizo la mkuu wa wilaya hiyo, Diwani wa kata ya Udekwa, Peter Mbosa alisema; “ni kweli baadhi yetu tunafanya shughuli za kilimo karibu na vyanzo vya maji, niseme tumesikia ushauri wa wataalamu na maagizo ya serikali, tukuahidi kwamba tunaanza kuondoka.”

Katika shindano la tuzo hiyo mwaka 2016/2017, wilaya ya Kilolo ilitoa mshindi wa pili aliyeshinda kundi la upandaji na utunzaji wa miti ya asili na mshindi wa tatu katika kundi la uhamasishaji na uelimishaji jamii.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment