Friday, 1 September 2017

CHUMI AMWAGA MISAADA KWA WANAFUNZI WALEMAVU MAFINGA

MBUNGE wa Jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi juzi amewakumbuka tena wanafunzi walemavu wanaosoma shule ya msingi mchanganyiko Makalala ya mjini Mafinga, safari hii akitoa msaada wa kofia, miwani, mafuta na vifaa mbalimbali kwa wanafunzi wenye ulemavu wa ngozi (Albino).

Pamoja na misaada yake ya mara kwa mara kwa wanafunzi hao, mbunge huyo amekuwa mstari wa mbele kuzitafutia ufumbuzi kero mbalimbali zinazoikabili shule hiyo yenye wanafunzi 82 walemavu, wakiwemo 24 wasioona.

Wakati mbunge huyo akiingia madarakani Novemba 2015, shule hiyo ilikuwa na mwalimu mmoja, lakini hivi sasa ina walimu tisa, kati yao saba ni kwa ajili ya wanafunzi wasioona na wawili wenye ulemavu wa akili.

Mkuu wa shule hiyo, Emanuel Ngombale alizitaja changamoto zingine zinazoikabili shule hiyo kuwa ni pamoja na uhaba wa mabweni, maji na vyakula maalumu kwa ajili ya wanafunzi hao.

Zingine ni upungufu wa vifaa vya kufundishia, walimu, vitanda, magodoro haina gari la shule, na kwa upande wa wanafunzi hao wana uhaba wa mavazi, viatu na mahitaji mengine yao mengine ya msingi.

Alisema pamoja na kwamba serikali imekuwa ikitekeleza wajibu wake wa kupeleka chakula shuleni hapa (unga na maharage), wanafunzi hao wanahitaji vyakula mchanganyiko ili kukidhi mahitaji yao ya mwili na akili.

Katika kushughulikia changamoto hizo, Machi 14, 2016 mbunge huyo alimpeleka shuleni hapo Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi (Utumishi na Utawala Bora), Selemani Jaffo ambaye aliiagiza halmashauri ya mji Mafinga kutumia vyanzo vyake vya mapato kujenga mabweni mapya kwa ajili ya wanafunzi hao.

“Agizo hilo limeanza kutekelezwa na bweni moja la wavulana lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 36 limekwishajengwa. Ni matarajio yetu serikali itatoa pia fedha kwa ajili ya ujenzi wa bweni jipya la wasichana,” alisema Chumi.

Julai 30, 2016 mbunge huyo alimpeleka shuleni hapo Balozi wa Korea nchini, Song Geum Young aliyekuwa ameambatana na taaisi ya kimataifa ya World Share iliyoahidi kushughulikia tatizo la maji, hata hivyo ahadi hiyo haijaanza kutekelezwa.

Akikabidhi msaada huo kwa wanafunzi wenye ualbino, Chumi aliyekuwa ameambata na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Charles Makoga na baadhi ya madiwani aliwaomba wadau wengine kujitokeza kupunguza makali ya changamoto zinazoikabili shule hiyo.

“Watoto hawa wana mahitaji mengi, na baadhi yake ni ya gharama kubwa, kwahiyo ni jambo la kheri pale wadau mbalimbali wa maendeleo wanapojitokeza na kuwasaidia ili nao waweze kukamilisha ndoto zao za kupata elimu wanayoihitaji,” alisema.


Shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1954 ilianza kwa kupokea wanafunzi wasioona mwaka 1974 kabla ya kuanza kuchukua watoto wenye mtindio wa ubongo na walemavu wengine miaka iliyofuata.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment