Tuesday, 29 August 2017

WAKUU WA MIKOA YA NYANDA ZA JUU KUSINI WATALII HIFADHI YA TAIFA RUAHA


WAKUU wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wametembelea kwa siku mbili Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwa mara ya kwanza wakiwa pamoja na kusema wanashangaa kuona hifadhi hiyo kubwa kuliko zote nchini inavyochelewa kuleta tija kwa utalii wa kusini na maendeleo ya Taifa.

Walitembela hifadhi hiyo kwa uratibu wa Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST) ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maonesho ya utalii ya Karibu Kusini yatakayofanyika kwa mara ya pili kati ya Septemba 29 na Oktoba 2, mwaka huu, mjini Iringa.

Kwa mara ya kwanza maonesho hayo yaliyokwenda sambamba na maadhimisho ya siku ya Utalii Duniani Kitaifa, yalifanyika mjini Iringa kati ya Novemba 25 na 29, mwaka jana.

“Ukienda Kaskazini, utashangaa kukutana na misururu ya magari yenye watalii wengi wa nje na ndani yakielekea katika hifadhi mbalimbali za mikoa hiyo, lakini hali hiyo ni tofauti kabisa katika hifadhi hiyo ya Ruaha na vivutio vingine vya kusini” alisema Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Luteni Mstaafu Chiku Galawa.

Katika ziara hiyo ambayo haikuhudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makala, Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka alisema mikoa ya kusini ina deni kubwa la kuitangaza hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

“Ni mara yangu ya kwanza kutembelea hifadhi hii, hifadhi ni kubwa kweli kweli na ina wanyama wa kila aina na vivutio vingine vingi, lakini ukubwa wake hauonekani kwasababu haijatangazwa,” alisema.

Alisema kama hifadhi hiyo ikitangazwa vyema na changamoto zake zikiwemo za miundombinu ya barabara zikashughulikiwa ipasavyo, inaweza kuwa hifadhi ya kwanza nchini kwa kuingiza fedha nyingi zikiwemo za kigeni.

Kwa kuzingatia kwamba mkoa wa Iringa ulitangazwa kuwa lango la utalii wa mikoa ya kusini, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema walipeleka ombi maalumu kwa Rais Dk John Magufuli kwa ajili ya upanuzi wa uwanja wa ndege wa Nduli mjini Iringa na kujenga barabara ya Iringa-Ruaha kwa kiwango cha lami.

 “Ni imani yetu maombi hayo yatafanyiwa kazi, na kwa upande wetu tuna wajibu wa kuunganisha nguvu na tuwe na matumizi ya lugha ya pamoja wakati tukinadi utalii wa kusini, ,” alisema huku akiweka tahadhari kama kila mkoa utafanya shughuli hiyo kivyake.

Awali Mratibu wa SPANEST, Godwell Ole Meing’ataki alisema Tanzania ni nchi ya pili duniani kwa kuwa na vivutio vya utalii lakini inachelewa kunufaika na rasilimali hizo kwasababu ya changamoto mbalimbali, nyingi zikiwa ni zile zilizoko nje ya vivutio hivyo.

“Tuna vivutio, lakini tuna changamoto ya usafiri na wasafirishaji watalii, sehemu za kulala wageni, huduma za vyakula na zingine muhimu kwa wageni, taarifa za vivutio vya utalii, huduma ya kuongoza watalii na zinginezo muhimu kwa wageni,” alisema.

Katika kipindi cha miaka minne ya utekelezaji wake, Meing’ataki alisema SPANEST imefanya mambo mengi katika mikoa hiyo yakakayosaidia kuboresha mazingira wezeshi kwa  shughuli za uhifadhi na utalii ili zifanyike kwa viwango vya kuridhisha.

Ikiwa imedhamiria kuboresha sekta ya utalii katika mikoa ya kusini, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Utalii nchini,  Phillip Chitaunga alisema serikali ipo katika hatua za mwisho za kuanza kutekeleza mradi mkubwa wa kuendelea utalii kusini utakaofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Kwa kupitia mradi huo, Chitaunga alisema miundombinu ya hifadhi itaboreshwa, uwekezaji utaimarishwa na kutakuwa na kituo kikubwa cha kutangaza utalii kusini kitakachojengwa mjini Iringa.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment