Monday, 7 August 2017

WAKULIMA WA NYANYA WAPATA HOFU YA SOKO

Image result for mashamba ya nyanya

WAKULIMA wa nyanya wilayani Iringa wamelalamika kupata hasara baada ya sehemu kubwa ya zao hilo linalolimwa mwaka huu kuoza likiwa shambani kwasababu ya ukosefu wa masoko.

Mmoja wa wakulima aliyekumbwa na hasara hiyo ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Steven Mhapa aliyesema zaidi ya tenga 600 za nyanya zimeoza shambani kwake Nzihi ikiwa ni matokeo ya kukosa soko.

Mhapa alisema pamoja na kwamba zao hilo liliporomoka bei hadi tenga moja kuuzwa kwa Sh 3,000 badala ya zaidi ya Sh 20,000, soko la zao hilo limeendelea kuwa tatizo na kuwakatisha tamaa wakulima wengi wakiwemo wale wapya wanaoichangamkia fursa hiyo.

Pamoja na kwamba wilaya ya Iringa ina viwanda vitatu vinavyosindika zao hilo, Mhapa alisema havijaweza kumkomboa mkulima kwani navyo vinanunua kwa bei ya kutupwa.

“Watu wengi wanatumia fursa ya kilimo kujaribu kubadili maisha yao, lakini hali ya soko ya mazao mbalimbali tunayozalisha mara kwa mara imekuwa na changamoto ya bei,” alisema.

Akizungumzia malalamiko ya wakulima wa zao hilo kwenye kikao cha wadau wa sekta ya biashara wanaounda Mtandao Unaotafiti Kero za Biashara (Multi Actors Integration-MAI) Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alisema bei ya zao hilo itaimarika kama viwanda vya kusindika mazao ya mbogamboga vitaongezeka.

“Ni kweli Iringa tuna viwanda vitatu lakini havikidhi mahitaji ya wakulima. Kwahiyo kuna haja ya kuendelea kuwahamasisha wadau kujenga viwanda vingi kama inavyoshauriwa na Mheshimiwa Rais,” alisema.

Kwa upande mwingine Kasesela alisema madalali wa biashara hiyo ya nyanya wanachangia kurudisha nyuma mapato ya wakulima.

“Utafiti wetu unaonesha wanaofaidika zaidi na mazao yanayolimwa na mkulima ni madalali, kwasababu dalali akinunua kwa mkulima tenga moja la nyanya kwa Sh 3,000 yeye atauza zaidi ya mara tatu ya bei hiyo,” alisema.

Ili kuondokana na hali hiyo, Kasesela aliwashauri wenye viwanda kujenga vituo vya kununulia nyanya katika maeneo yanayolimwa zao hilo ili mkulima aweze kupata bei stahiki kutoka kiwandani na kwa wateja wengine.

“Lakini nawashauri pia wakulima waangalie uwezekano wa kulima zao hilo kwa mzunguko ili kuimarisha soko lake badala ya wote kulima kwa wakati mmoja jambo linaloporomosha soko wakati wa mavuno kwasababu ya wingi wake,” alisema.

Awali Mwenyekiti wa MAI, Lucas Mwakabungu aliipongeza serikali kwa kusikia kilio chao kwa kufuta kodi na tozo mbalimbali za mazao ya kilimo zilizokuwa zinawaongezea wakulima mzigo wa uzalishaji na hivyo kupunguza tija.

Alisema MAI inayoundwa na wadau wa sekta ya biashara wa mikoa ya Iringa, Morogoro, Mbeya, Njombe na Ruvuma ambayo ipo katika Ukanda wa Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) inafanya kazi ya kutafiti kero za kibiashara katika mikoa hiyo na kuziwasilisha serikalini kwa utekelezaji.

Pamoja na mikoa hiyo inayowakilishwa na chemba za TCCIA, wadau wengine wa MAI ni Umoja wa Vyuo Vikuu Nchini, vyombo vya habari na washirika wengine katika sekta ya biashara na kilimo likiwemo Jukwaa la Wadau wa Kilimo Tanzania (ANSAF), taasisi inayojihusisha na kilimo cha mbogamboga, matunda na maua nchini (TAHA) na mpango wa SAGCOT wenyewe.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment