Thursday, 10 August 2017

TANZANIA HATARINI KUBAKI NA HIFADHI MBILIImage result for Dk Kikoti

Mtaalam na Mtafiti wa Tembo, Dkt Alfred Kikoti amesema  Tanzania  ipo katika hatari ya kubakiwa na hifadhi za wanyamapori mbili kati ya 16 na mapori ya akiba yaliyopo ifikapo mwaka 2050 kama hatua za haraka hazitachukuliwa kuzinusuru.

Dk Kikoti aliyasema hayo hivikaribuni mjini Dodoma kwenye kikao cha kamati ya ufundi kilichokuwa kikipokea taarifa ya shughuli zilizofanywa na Mradi  wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST) tangu uanze kutekelezwa miaka minne iliyopita katika mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe, Dodoma na Singida. 

Kamati hiyo ilipendekeza pia namna shughuli za mradi huo zinazoendelea zitakavyotekelezwa na wadau wengine wa sekta ya uhifadhi na utalii baada ya mradi huo uliobakisha miezi sita ya utekelezaji wake, kufikia tamati Desemba mwaka huu.

Dk Kikoti alisema ongezeko la watu limezifanya hifadhi nyingi zizingirwe na makazi ya watu na hivyo kuharibu njia za wanyama (ushoroba) lakini pia ujangili, uharibifu wa mazingira pamoja na mabadiliko ya tabia nchi kwa pamoja vinahatarisha uhai wa viumbe hai katika hifadhi mbalimbali nchini.

Alisema wanyama kama walivyo binadamu wanahitaji uhuru wa kutawala mazingira yao ikiwa ni pamoja na kuhama kutoka hifadhi moja kwenda nyingine kwasababu ya mabadiliko ya hali ya hewa, lakini kwa bahati mbaya njia zao zimeingiliwa na shughuli za binadamu.

“Zipo hifadhi kama ya Sadani ambazo zinaendelea kuzungukwa na makazi ya watu hatua itakayosababisha wanyama waliopo katika hifadhi hiyo washindwe kuhamia sehemu nyingine pale hali ya hewa katika hifadhi hiyo inapobadilika. Madhara yake ni kwamba wanyama hao watakufa na hifadhi hizo kubaki historia,” alisema. 

Kwa mtazamo wake, Dk Kikoti alisema kama hayo yote hayatafanyiwa kazi hifadhi pekee zinazoweza kunusurika na hali hiyo ni ya Ruaha Rungwa na pori la akiba la Selous kwasababu ya kubwa na mazingira yake.

Alisema miaka mingi iliyopita lilikuwa si jambo la ajabu kuona wanyamapori wakipita jirani na maeneo ya watu kwasababu kulikuwa na njia zao ambazo hivisasa hazipo.

Alisema kupungua kwa vitendo vya ujangili vimewafanya wanyama wakiwemo Tembo waanze kuzikumbuka njia zao kama ilivyojidhihirisha hivikaribuni katika maeneo ya miji mbalimbali.

“Hivikaribuni tuliona Tembo karibu na Chuo Kikuu cha Dodoma mjini Dodoma na wakijaribu kupita katika miji mingine kama Ikungi na Kondoa; msifikiri walipotea njia, wanyama hao wamezikumbuka njia zao baada ya usalama wao kuimarika, kwa bahati mbaya wamekuta njia hizo zimeingiliwa na shughuli za binadamu na katika mazingira hayo wanaweza kuuawa,” alisema.

Mratibu wa SPANEST, Godwell Ole Meing’ataki alisema ni vizuri wananchi wakapewa elimu ya hatua zisizo na madhara wanazopaswa kuchukua pindi wakiwaona wanyama katika maeneo yao.

Alisema bila elimu hiyo, ipo hatari kwa wanyama hao kuuawa au kuleta madhara makubwa kwa jamii na kasisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki kuhifadhi maeneo yaliyohifadhiwa pamoja na shoroba za wanyama


Reactions:

0 comments:

Post a Comment