Monday, 14 August 2017

MAGHEMBE AFUTA MIKATABA YA UWINDAJI, AVUNJA BODI YA MBOMIPAWAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe ameivunja bodi ya Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Tarafa ya Idodi na Pawaga (Mbomipa) pamoja na kufuta mikataba ya kampuni mbili zinazoendesha shughuli za uwindaji wa kitalii katika eneo hilo.

Mbomipa ni eneo la hifadhi ya jamii ya wanyamapori linalopakana na hifadhi ya Taifa ya Ruaha, wilayani Iringa mkoani Iringa lenye wanyamapori wengi wanaoingia na kutoka katika hifadhi hiyo linaloundwa na vijiji 21 vya tarafa hizo mbili.

Bodi iliyovunjwa inaundwa na Mwenyekiti Zabron Luvinga na Steven Nyandongo, Alban Lutambi, Mawazo Malembeka na Denis Ngede ambao ni wajumbe; na kampuni zilizofutiwa mikataba ni Kilombero North Safaris Ltd na Mkwawa Hunting Safaris Ltd.

Wakati mmiliki wa kampuni ya Mkwawa Hunting Safaris Ltd Ahamed Huwel alisema amepokea bila kinyongo chochote uamuzi huo wa waziri alioutangaza juzi mbele ya wanajumuiya hiyo katika kijiji cha Tungamalenga, mmiliki wa Kilombero North Safaris Ltd, Acram Aziz hakupatikana kuzungumzia uamuzi huo.

Hatua ya Waziri Maghembe kuvunja bodi na kufuta mikataba ya jumuiya hiyo na kampuni hizo imekuja kwa kuzingatia matokeo ya timu ya wataalamu aliyoiunda hivikaribuni kuchunguza dosari na malalamiko ya uendeshaji wa taasisi hiyo na kubaini mapungufu makubwa ya kisheria na kiutendaji.

“Kwanza Katiba inayotumiwa na jumuiya hii inakinzana na sheria za wanyamapori, kanuni za uwindaji wa wanyamapori na utalii wa kupiga picha; lakini pia bodi haiko pamoja, kila upande una mwekezaji wake,” alisema.

Kwa mazingira hayo, waziri huyo alisema katiba ya jumuiya hiyo inatakiwa kufumuliwa upya na baada ya hapo bodi mpya uindwe katika mchakato alioagiza uwe umakamilika kabla ya Oktoba mwaka huu na baada ya hapo shughuli ya kutafuta wawekezaji ianze upya.

Profesa Maghembe alisema eneo la jumuiya hiyo lina utajiri mkubwa lakini akashangaa kuambiwa kwamba wana jumuiya hawana wanachopata kutokana na uwekezaji unaofanywa eneo hilo, jumuiya haina uwezo wa kulipa mishahara watumishi na walinzi wake na inashindwa kufanya shughuli zake mbalimbali za kiofisi na matengenezo ya vifaa na gari lao yamekuwa yakifanywa kwa kupitisha bakuri.

Awali katibu wa Mbomipa, Josephat Kisanyagi alisema jumuiya imekuwa katika mtikisiko mkubwa wa kukosa mapato kutoka kwa wawekezaji wake katika kipindi chaJulai 2016 hadi sasa.

“Kukosekana kwa mapato hayo kumesimamisha shughuli muhimu za jumuiya hiyo huku viongozi na walinzi wanaofanya kazi ya doria katika eneo hilo la Mbomipa wakikosa mishahara na stahiki zao,” alisema.

Akionekara kukerwa na kile kinachoendelea ndani ya jumuiya hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza alisema; “hakuna kijiji hata kimoja kati ya vijiji 21 vinavyounda jumuiya hiyo kinachoweza kusema kimenufaika na uwepo wa Mbomipa.”

Masenza alisema katika jumuiya hiyo pamekuwepo na migongano isiyokwisha na utapeli uliokithiri ambao sehemu yake kubwa ulifanywa na bodi zilizopita kana kwamba Mbomipa ilikuwa mali yao.

“Kwa maneno mepesi bodi ilipewa mamlaka na madaraka makubwa juu ya Mbomipa kuliko inavyotakiwa, kumekuwa na kufukuzana na kuchaguana mara kwa mara kwasababu baadhi ya watu waliokuwa wakipata uongozi waliomba uongozi ili kukidhi maslai yao,” alisema.

Akiahidi kuyasimamia maamuzi hayo ya waziri, Masenza aliwageukia pia baadhi ya wawekezaji katika eneo hilo la Mbomipa akisema wamekuwa matapeli na hivyo kuifanya jumuiya hiyo ifike hapo ilipo na kugeuka kuwa ombaomba.

Baada ya taarifa hiyo ya mkuu wa mkoa, Profesa Maghembe aliiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanya uchunguzi wa mapato na matumizi ya jumuiya hiyo ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa watu watakaobainika waliitumia kujinufaisha.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment