Sunday, 27 August 2017

LIPULI YAHITAJI MILIONI 800 KUSHIRIKI VYEMA LIGI KUU


IKISHUKA dimbani hii leo kumenyana na Yanga SC katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara iliyoanza kutimua vumbi jana katika viwanja mbalimbali vya soka nchini, Lipuli FC ya mjini Iringa inahitaji zaidi ya Sh Milioni 800 ili iweze kushiriki vyema kinyang’anyiro hicho.

Lipuli FC imerejea katika ligi hiyo ikiwa ni miaka 17 tangu iliposhuka daraja na baada ya hapo mkoa wa Iringa kukosa timu nyingine iliyofanikiwa kucheza ligi hiyo.

Kwa kupitia Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza, hivikaribuni klabu hiyo iliandaa harambee ya kuichangia katika tukio lililokwenda sambamba na kukitambulisha kikosi cha timu hiyo na kula nacho chakula cha pamoja.

Akizungumza katika harambee hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango na Fedha, July Sawani alisema; “Kiasi hicho cha fedha kinahitajika kwa ajili ya kuiweka kambini timu hiyo, usafiri, posho na mishahara ya wachezaji na maafisa mbalimbali wa timu hiyo.”

Akiendesha harembee hiyo ambayo hata hivyo kiasi cha fedha kilichapatikana hakikutangazwa kwa kuwa baadhi ya wadau hawakuwa wamefikiwa ndani ya muda muafaka, Mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela aliwaomba wakazi wa manispaa ya Iringa na mkoa wa Iringa kwa ujumla wake kuifanya timu hiyo kama mtoto wao anayeweza kuchangia kusukuma gurudumu la maendeleo ya soka na mkoa wa Iringa.

Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdalla alisema kazi ya kuilinda timu hiyo ni ya kila mwana Iringa baada ya juhudi za muda mrefu za kuipandisha daraja kufanikiwa.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Jamuhuri William ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Mufindi alisema serikali ya mkoa wa Iringa itaendelea kuwa pamoja na timu hiyo kwa kuwa inajivunia uwepo wake katika ligi hiyo.

“Tunajua ghamara za kuendesha timu ya ligi kuu ilivyokuwaba, lakini pia tunajua kwamba timu haiwezi kuendeshwa kwa mapato ya mlango nay a udhamini pekee yake, kwahiyo ni muhimu tukawaomba wadau watusaidie. Ahadi ya serikali ya mkoa wa Iringa ni kusaidia kupata wadau hao,” alisema.

Msemaji wa Lipuli FC, Clement Sanga aliwataja wachezaji wanaounda kikosi cha timu hiyo kinachonolewa na Seleman Matolla kuwa ni pamoja na Alli Mtoni, Mohamed Yusuph, Tola Mwangonela, Ramadhani Madebe, Fadhili Butam, Mervyn Alistotle, Husein Dumba, Zamoyoni Pangapanga na Joseph Owino.

Wengine ni Samwel Nkomola, Moka Msafiri, Emannuel Kichiba, Mussa Ngunda, Fredy Tangalo, Doto Kayombo, Martin Kazila, Malimi Busungu, Omega Kabuje, Salum Machaku, Lambela Ruben, Ahamed Manzi, Kwasi Asante, Paulo Ngelema, Mussa Chibwabwa, Novatus Lufunga, Seif Rashid, Aghaton Mkwando na Waziri Hussein.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment