Tuesday, 8 August 2017

KILOLO YANG'ARA NANENANE MBEYA


WADAU wa maendeleo ya wilaya ya Kilolo wamempongeza mkuu wa wilaya hiyo, Asia Abdallah baada ya halmashauri yake kung’ara katika maonesho ya kilimo  na sherehe za wakulima ya nanenane 2017 ambayo katika kanda ya Nyanda za Juu Kusini, hufanyika jijini Mbeya.

Katika maonesho hayo yaliyofanyika leo Agosti 8, jijini humo, halmashauri ya wilaya ya Kilolo imekuwa mshindi wa tatu wa kanda katika kundi la halmashauri.

Kanda hiyo inaundwa na mikoa ya Iringa, Mbeya, Ruvuma, Rukwa, Katavi na Songwe.

Baadhi ya wananchi waliohojiwa akiwemo Afisa Mifugo wa Wilaya hiyo, Dk Mwingira; walisema ushindi huo ni zawadi kwa mkuu wa wilaya huyo ambaye siku zote amekuwa akiwahimiza wananchi wa wilaya hiyo kuongeza tija katika shughuli zao za kilimo ili wainue vipato vyao, wilaya na Taifa kwa ujumla.

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo alipeleka pongezi kwa wananchi na viongozi wote wa wilaya hiyo akisema juhudi zao katika sekta hiyo zimewafanya watambulike kikanda na kitaifa pia.

“Kilimo ndio shughuli kuu ya uchumi katika wilaya yetu. Tunalima mazao ya chakula, biashara, matunda na mbogamboga za aina mbalimbali na kwa pamoja shughuli hizo zinachangia kwa kiasi kikubwa kuinua kipato cha wilaya na wananchi wake. Kimsingi tunastahili ushindi huo,” alisema.

Pamoja na ushindi huo, Asia alisema kiu yao ni kuona halmashauri yao inashika nafasi ya kwanza katika mashindano yajayo pamoja na kwamba wanatambua ushindani mkali uliopo.

“ Tunataka tuwe namba moja , sifa na uwezo huo tunao japokuwa tunajua ushindani uliopo na hasa kwa kuzingatia kwamba wilaya zote za mikoa ya nyanda za juu kusini zinasifika kwa ufugaji na kilimo cha mazao mbalimbali,” alisema.

Aliwaagiza viongozi wa halmashauri yake kutengeneza mazingira yatakayowawezesha kukwea hadi nafasi ya kwanza katika maonesho ya mwakani.

“Kilolo ina fursa nyingi sana za kilimo, ina maeneo makubwa na mazuri ya uwekezaji, ina hali ya hewa nzuri na mvua za uhakika. Tukiyatumia haya vizuri kilimo wilayani Kilolo kitatuvusha,” alisema.

Kwa kupitia ofisi yake ya mkuu wa wilaya, aliahidi kushirikiana na uongozi wa halmashauri hiyo kuboresha pale wanapoonekana wanakwama ili azma yao ya kuwa namba moja ifikiwe.

Kwa upande wake mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kilolo, Aloyce Kwezi alisema  halmashauri ina mikakati mingi itakayowezesha sekta ya kilimo wilayani humi kuimarika na kuwa yenye viwango vya hali ya juu.

“Niwakaribishe wadau wenye nia ya kuwekeza katika sekta hii kujitokeza kwani wilaya yetu ina maeneo mengi na mazuri kwa ajili ya shughuli hiyo lakini hayatumiki kwa shughuli hiyo,” alisema.Reactions:

0 comments:

Post a Comment