Sunday, 27 August 2017

ILULA WAPAMBANA KUMALIZA TATIZO LA MGAO WA MAJI


HUDUMA ya maji katika Mji Mdogo wa Ilula, wilayani Kilolo mkoani Iringa imeendelea kutolewa kwa mgao kwa miaka 10 sasa licha ya juhudi za serikali zilizotekelezwa kupunguza ukali wa upatikanaji wa huduma hiyo.

Akitoa taarifa ya hali ya huduma hiyo kwa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Iringa iliyotembelea mji huo juzi kujionea utekelezaji wa mradi mpya wa maji wa Mgombezi, Meneja wa Mamlaka ya Maji Ilula Enock Ngoyinde alisema mahitaji ya maji kwasasa katika mji huo ni mita za ujazo 2,687 kwa siku.

“Kwa sasa Mamlaka ya Maji Ilula inatoa huduma yake kupitia vyanzo viwili vya maji vya mtiririko ambavyo ni Ilomba na Idumule. Kwa ujumla vyanzo hivi kwasasa vina wastani wa uzalishaji wa maji wa mita za ujazo 1,142 tu,” alisema.

Alisema hali imesababisha huduma hiyo itolewe kwa mgao wa wastani wa saa 6 hadi 8 kwa eneo moja kwa mzunguko wa siku moja kila baada ya siku saba kwa wiki katika eneo lote lenye mtandao wa bomba.

“Mamlaka hii inayotakiwa kuhudumia watu 45,486 ina jumla ya mtandao wa mabomba wenye urefu wa Kilometa 51.35 kwa eneo lote la uhendeshaji wa huduma ya maji kwa sasa,” alisema.

Alisema kwa mzunguko huo wa mgao wa maji idadi ya wakazi wanaopata huduma ya maji kwasasa ni 18,790 ya wakazi wote.

Licha ya changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji, Ngoyinde alisema kwa kupitia program ya Sekta ya Maendeleo ya Miradi ya Maji (WSDP), serikali imekwishafanya usanifu wa kuboresha huduma ya maji katika mji huo kwa kutumia vyanzo vipya vya maji vya Mgombezi, Madisi na Kihoroto utakaogharimu zaidi ya Sh Bilioni 14.

Kwa kupitia Wizara ya Maji, mwaka wa fedha wa 2016/2017 serikali ilitenga kiasi cha Sh Milioni 800 ili kuanza utekelezaji wa mpango wa kuboresha huduma hiyo kupitia chanzo kipya cha Mgombezi kitakachokuwa na uwezo wa kuzalisha mita za ujazo za maji 5,184 kwa siku pindi mradi huo utakapokamilika.

Akipokea taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa CCM Mkoa wa Iringa, Ephraim Mhekwa aliyekuwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza na Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Asia Abdalla alisema kama chama wataihimiza serikali kuendelea kuzipatia ufumbuzi kero za wananchi.

Ili kuifanikisha miradi mipya ya maji Mkuu wa Mkoa wa Iringa aliwataka wananchi wanaofanya shughuli zao karibu na vyanzo hivyo kuondoka huku mkuu wa wilaya hiyo akiahidi kulifanyia kazi agizo hilo.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment