Thursday, 31 August 2017

FIGISUFIGISU YA KITOVU CHA UTALII KUSINI YAMALIZWA


WIZARA ya Maliasili na Utalii imetanzua mkanganyiko wa mkoa utakaokuwa kitovu na lango la utalii kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini baada ya hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amos Makala kunukuliwa akiutangazia umma kwamba mkoa wake ndio utakaobeba jukumu hilo.

Akiwa katika kikao chake na viongozi wa mkoa huo Juni 21, mwaka huu Makala aliyekuwa akitoa tathmini ya mwaka mmoja uliopita ya uongozi wake alitangaza mikakati ya kuifanya Mbeya kuwa lango la utalii na uchumi kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Katika kikao hicho kilichofanyika ofisini kwake jijini Mbeya mkuu wa mkoa huyo alitaja sababu za mkoa huo kuwa lango la utalii na uchumi wa mikoa hiyo kuwa ni pamoja na uwepo wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Songwe, bandari ya Kiwira wilayani Kyela na kuwepo kwa barabara zinazounganisha Tanzania na nchi za Malawi, Zambia na nchi za ukanda wa Afrika Kusini.

Tamko hilo la Makala likamuibua Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza ambaye katika kikao cha maandalizi ya maonesho ya utalii ya Karibu Kusini yanayofanyikia mjini Iringa kila mwaka toka yaanzishwe mwaka jana aliitaka wizara itoe ufafanuzi kwa kuwa ilikwishautangaza mkoa wa Iringa kuwa kitovu na lango la utalii wa mikoa ya kusini.

“Kuna mahali naona kama hapaendi sawa, wizara ya maliasili na utalii ilikwishatoa maelekezo, ni vizuri ikawa wazi katika hili ili kutowachanganya wananchi,” alisema.

“Na kama kuna mabadiliko yoyote yalifanywa kinyemela nitalazimika kuwasiliana na waziri mwenye dhamana na wizara hiyo ili yale yaliyoelekezwa na wizara yazingatiwe,” alisema katika kikao hicho kilichofanyika mjini Iringa juzi kikihusisha wawakilishi mbalimbali kutoka mikoa ya kanda hiyo.

Akitoa maelekezo ya wizara Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Utalii nchini,  Phillip Chitaunga alisema serikali ilikwishautangaza mkoa wa Iringa kuwa kitovu na lango la utalii wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini katika jitihada zake za kuendeleza utalii katika mikoa hiyo.

“Maamuzi hayo hayakufanywa kienyeji, Mkoa wa Iringa ulipewa hadhi hiyo baada ya wizara ya maliasili na utalii kufanya utafiti. Naomba hili likae sawasawa,” alisema.

Alisema baada ya utafiti huo, wizara ilikuja na ramani kuu (master plan) yenye michoro inayoonesha kwanini Iringa imepewa hadhi hiyo na ndiyo inayostahili kuwa lango la utalii kwa mikoa hiyo.

Ikiwa imedhamiria kuboresha sekta ya utalii katika mikoa ya kusini, Chitaunga alisema serikali ipo katika hatua za mwisho za kuanza kutekeleza mradi mkubwa wa kuendelea utalii kusini utakaofadhiliwa na Benki ya Dunia.

Kwa kupitia mradi huo, Chitaunga alisema miundombinu ya hifadhi itaboreshwa, uwekezaji utaimarishwa na kutakuwa na kituo kikubwa cha kutangaza utalii kusini kitakachojengwa mjini Iringa.

Awali Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST), Godwell Ole Meing’ataki alisema Tanzania ni nchi ya pili duniani kwa kuwa na vivutio vya utalii lakini inachelewa kunufaika na rasilimali hizo kwasababu ya changamoto mbalimbali, nyingi zikiwa ni zile zilizoko nje ya vivutio hivyo.

“Tuna vivutio, lakini tuna changamoto ya usafiri na wasafirishaji watalii, sehemu za kulala wageni, huduma za vyakula na zingine muhimu kwa wageni, taarifa za vivutio vya utalii, huduma ya kuongoza watalii na zinginezo muhimu kwa wageni,” alisema.


Katika kipindi cha miaka minne ya utekelezaji wake, Meing’ataki alisema SPANEST imefanya mambo mengi katika mikoa hiyo  ya kusini yakakayosaidia kuboresha mazingira wezeshi kwa  shughuli za uhifadhi na utalii ili zifanyike kwa viwango vya kuridhisha.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment