Thursday, 31 August 2017

CHUMI AKABIDHI MSAADA WA WA KUWAIT KWA AKINA MAMA WALIOJIFUNGUA MAFINGA


UBALOZI wa Kuwait nchini umemtoa msaada wa beseni na vifaa mbalimbali kwa ajili ya matumizi ya watoto wachanga 100 waliozaliwa katika hospitali ya wilaya ya Mufindi, mjini Mafinga hivikaribuni.

Vifaa hivyo ni pamoja na mavazi ya watoto kwa ajili ya kujisitiri na baridi, mafuta, vifaa vya kuwasafishia na kuwasaidia wanaponyonya.

Msaada huo wenye thamani ya Sh Milioni 4 ulikabidhiwa kwa akina mama wa watoto hao hospitalini hapo jana na Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi.

Akikabidhi msaada huo, Chumi aliushukuru ubalozi wa Kuwaita akisema; “Tumetengeneza urafiki wa kudumu utakaowawezesha wananchi wa Jimbo la Mafinga Mjini na wilaya ya Mufindi kwa ujumla wake kunufaika na misaada mbalimbali tutakayokuwa tukiomba na kupewa.”

Kwa kupitia urafiki huo, Chumi alisema baada ya kuomba na kupewa  vifaa hivyo kwa ajili ya watoto, amekwishawasilisha maombi mengine kwa ubalozi huo yatakayosaidia kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya mji huo.

“Marafiki hawa wametuahidi pia kutupatia msaada wa vifaa vya maabara lakini pia wameonesha nia ya kujenga chuo cha ualimu mjini Mafinga,” alisema.

Akishukuru kwa msaada huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Charles Makoga alimpongeza Chumi akisema tangu awe mbunge amekuwa akijali maisha ya watu na kushughulikia kwa nguvu zake zote changamoto za huduma za afya.

“Ametafuta na kukabidhi vifaa tiba na dawa za aina mbalimbali kwa hospitali hii na kipaumbele chake kimekuwa kwa akina mama akiamini mama ni kila kitu,” alisema.

Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga, Dk Innocent Mhagama alisema vifaa hivyo kwa ajili ya kulea watoto katika hatua za mwanzo umepokelewa kwa mikono miwili na akina mama hao kwakuwa umewapunguzia gharama.

“Tunafahamu kwamba sio kila mama anayejifungua anakuwa na uwezo wa kupata au kununu vifaa hivyo kwa wakati, kwahiyo msaada huu ni zawadi kubwa kwao,” alisema.


Akishukuru kwa niaba ya akina mama hao, Olelia Lunyungu alisema; “msaada huu utawafaa watoto wetu kwa kipindi kirefu, tumshukuru mbunge kwa jitihada hizi na tunamuombea kwa Mungu ampe maisha marefu,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment