Thursday, 24 August 2017

CHADEMA IRINGA MJINI YAMNG'OA DIWANI MWINGINE BAADA YA WENGINE WATATU KUACHIA NGAZI


SIKU moja baada ya madiwani watatu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Iringa Mjini kutangaza kujivua uanachama wa chama hicho na kupoteza nafasi zao zote za uongozi; viongozi wa chama hicho wameibuka na kutangaza kumng'oa  diwani wao mwingine kwa tuhuma ya kuvunja katiba ya chama.

Diwani huyo wa viti maalumu Iringa Mjini, Lugano Mwanyingi anadaiwa kupoteza uanachama wachama hicho baada ya kufungua kesi dhidi ya mwanachama mwenzake jambo ambalo kwa mujibu wa katiba ya chama hicho limempotezea sifa ya uanachama.

Mwanyingi alifungua kesi hiyo mapema mwezi huu, baada ya kujeruhiwa kwa kipigo na mlinzi wa chama hicho aliyetajwa kwa jina la Samweli Nyanda anayetuhumiwa pia kumdhalilisha kijinsia kwa kumshikashika matiti na makalio wakati wa kikao cha Kamati ya Utendaji ya chama hicho jimbo la Iringa mjini kilichofanyika Agosti 3, mwaka huu.

Baada ya kipigo hicho diwani huyo alilazwa kwa wiki moja katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa kabla ya kuhamishiwa Muhimbili anakoendelea kupata matibabu kwa kile kilichoelezwa kujeruhiwa sana sehemu za mbavu.

Akitangaza uamuzi huo jana baada ya Mbunge wa Jimbo la Iringa Mch Peter Msigwa kuwatuhumu madiwani hao kununuliwa  na Chama cha Mapinduzi (CCM), Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa,  Alex Kimbe alisema diwani Mwanyingi anaungana na madiwani watatu waliotangaza kujivua uanachama, kupoteza sifa ya kuendelea kuwa mwanachama wa Chadema baada ya kumshitaki mwanachama mwenzake.

Madiwani hao watatu waliotangaza kujivua nyadhifa zao zote za uongozi wa kisiasa katika chama hicho na kujitoa uanachama ni pamoja na Baraka Kimata, Diwani wa Kata ya Kitwiru, Leah Mleleu na Husna Daudi, wote wa viti maalumu Iringa Mjini.

“Kwa hiyo nitakutana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa kujadili suala hili na baadaye nitamuandikia barua waziri mwenye dhamana kumpa taarifa ya madiwani hao ili achukue taratibu za kujaza nafasi hizo,” alisema huku akikiri pia kupokea barua za madiwani watatu waliotangaza kujihudhuru.

Awali Mchungaji Msigwa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini aliwaambia wanahabari kwamba kwa muda mrefu kulikuwepo na taarifa za madiwani hao kununuliwa na wapinzani wao wa kisiasa Chama cha Mapinduzi (CCM) na kujitoa kwao Chadema ni jambo lililotarajiwa.

“Hizo ni hila za wapinzani wetu, walianza Arumeru wakaenda Arusha na sasa wamekuja Iringa. Lakini niwaambie Chadema iko imara na itaendelea kuwa imara. Tutajaza nafasi za madiwani wa viti maalumu na katika kata ya Kitwiru tuna uhakika wa kushinda kwa kishindo,” alisema.

Akithibitisha taarifa ya Mchungaji Msigwa, Meya huyo alisema hivi karibuni madiwani hao walifanya vikao na mawakala wa biashara hiyo katika maenero mawili tofauti mjini Iringa na taarifa ya kilichojadiliwa na kukubaliwa katika vikao hivyo wanazo.

“Vikao hivyo vilivyofanyika kwa nyakati tofauti katika hoteli ya Ruaha International mjini Iringa na katika nyumba ya mwanasiasa mmoja wa mjini Iringa iliyopo eneo la Mshindo,” alisema na kumtaja mwanasiasa huyo  kwa jina moja la Ngwada.

Akiwatakia kheri ya maisha mapya huko waendako, Mchungaji Msigwa alionya kwamba kwamba kila chama kina taratibu na maadili yake na wanaozivunja ni lazima wachukuliwe hatua.

“Kama ambavyo CCM inavyofanya kwa makada wake wanaokutwa na makosa mbalimbali, hata Chadema inao utaratibu wake wa kushughulikia mambo kama hayo. Kwahiyo isionekane kawaida CCM inapowataja wasaliti wa chama chake lakini ikawa ajabu Chadema inapofanya hivyo, watu hao wapo katika kila chama,” alisema.

Akikanusha madai yaliyotolewa na madiwani hao kwamba ni mkandamizaji wa demokrasia ndani ya chama hicho, kiongozi asiyefuata katiba na anayeamua kifanyike kile anachotaka yeye, Mchungaji Msigwa alisema hajawahi kuwa juu ya katiba ya chama hicho na kwamba mambo yao yote yanaendeshwa kwa msingi wa katiba ya chama.

“Kwanini wanituhumu barabarani, kama wana ushahidi walipaswa kuleta malalamiko yao ndani ya chama, utaratibu huo wanaujua na hawakufanya hivyo. Huu ni mpango uliosukwa kuivuruga Chadema, wasidhani matusi yao yatawasaidia chochote katika Uchaguzi Mkuu wa 2020,” alisema Mchungaji Msigwa ambaye hivikaribuni alitangaza kuwania kwa mara ya tatu ubunge wa jimbo la Iringa Mjini katika uchaguzi mkuu ujao.

Naye Katibu wa Kanda ya Nyanda za Juu wa chama hicho, Emmnuel Masonga alisema chama kimepokea taarifa za madiwani hao kujitoa Chadema na kinawatakia maisha mema huko waendako lakini kimesikitishwa na taarifa za upotoshaji wanazozitoa.

“Wangekuwa ni watu wema wangefuata taratibu za kutoa malalamiko yao. Lakini hawakufanya hivyo na sisi tunachukulia kama huo ni mchezo wa kawaida wa siasa,” alisema.

Pamoja na hali ya kisiasa inayoendelea nchini hivisasa, kiongozi huyo alisema Chadema itaibuka mashujaa katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

“Tumebadili namna ya kuendesha siasa, watanzania walizoea siasa za mihemko, sasa hivi hatufanyi, na sio kwamba hatufanyi kwasababu Rais kazuia mikutano ya kisiasa, hapana, ila ni kwasababu tunaamini hatuwezi kutumia mbinu zile zile halafu katika mazingira ya sasa tukapata matokeo tofauti,” aliongeza Mchungaji Msigwa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Taifa.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment