Sunday, 27 August 2017

CHADEMA IRINGA MJINI WAMPA BIG UP MBUNGE RITTA KABATI


WENYEVITI wa mitaa mbalimbali ya mjini Iringa waliochaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2014 kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wameupongeza utaratibu unaotumiwa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Ritta Kabati (CCM) kusikiliza kero mbalimbali za wananchi

Mbunge huyo aliitisha kikao maalumu na wenyeviti wa mitaa 192 ya Jimbo la Iringa kilichoshirikisha wataalamu wa idara mbalimbali za halmashauri ya manispaa ya Iringa akilenga kusikiliza na kuzitafutia ufumbuzi kero mbalimbali zilizoko katika mitaa hiyo.

Pamoja na kukutana na wenyeviti hao, mbunge huyo amekuwa na utaratibu wa kukutana na makundi mbalimbali ya jamii katika jimbo hilo na majimbo mengine mkoani Iringa, na kupokea kero zao zikiwemo zile zinazotakiwa kuwakilishwa bungeni.

Mmoja wa wenyeviti hao aliyechaguliwa kupitia Chadema, Pascal Bella (mtaa wa Kidunda) alisema; “Nikupongeze na kukushukuru sana mbunge kwa kutuita, utaratibu huu umeanza kubadili ule mtazamo kwamba wenyeviti wa mitaa ni watu wa ovyo ovyo.”

Bella aliyewahi kuwa Katibu wa Chadema wa Mkoa wa Iringa, alisema viongozi wengi wamekuwa na nidhamu mbaya dhidi ya wenyeviti wa mitaa, wengi wao wakiwaona viongozi hao kama watu wasio na hadhi.

“Katika shughuli mbalimbali tunazofanya hatupewi uzito unaostahili, viongozi hawatambui kwamba sisi ndio viongozi wa kwanza wa ngazi ya msingi ya mwanachi,” alisema.

Bella alirusha madongo kwa mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ya Iringa, Dk William Mafwere na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela kwamba toka wateuliwe na Rais Dk John Magufuli hawajawahi kukutana na wenyeviti wa mitaa.

“Hii ni dosari kubwa na tunaomba Mbunge utufikishie taarifa kwa viongozi hao maana hatujui kwa ngazi ya mitaa wanahsuariana na nani kushughulikia changamoto za maendeleo,” alisema.

Alisema amani wanayoiona viongozi hao katika ngazi hizo za mitaa ni matokeo ya kazi zao wanazofanya kwa saa nyingi ambazo hazina ukadiriaji.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Kinegamgosi B, Mzee Kihongozi (Chedema) alisema; “pamoja na kazi kubwa tunayofanya, heshima na thamani ya wenyeviti wa mitaa ni ndogo na ndio maana wanapomaliza miaka yao mitano ya uongozi huwa hawaitwi kupewa mkono wa heri na wala hawapewi chochote.”

Kihongosi alihoji kama viongozi wengine wa kisiasa kama madiwani na wabunge wanastahiki nyingi, ikiwemo posho kubwa na kiinua mgongo, kwani wenyeviti wa mitaa hawapati hivyo vyote kabla na baada ya kumaliza muda wao.

“Kwa kuwa wenyeviti wa mitaa tunatazamwa kama viongozi tusio na heshima, pendekezo langu tupewe hata baiskeli kwa ajili ya kazi zetu lakini wakati tukimaliza muda wetu wa uongozi angalau tuklumbukwe hata kwa kiinua mgongo cha Sh Milioni 2,” alisema.

Mbali na posho wanayolipwa kila mwezi ambayo walisema ni ndogo na hawaipati kwa wakati (Sh 20,000) wenyeviti hao 192 walitaja kero mbalimbali zinazokwamisha utendaji wao na zile zinazochelewesha maendeleo ya wananchi katika maeneo yao.


Baadhi ya kero walizotaja ni pamoja na miundombinu mibovu ya barabara hasa wakati wa mvua, ukosefu wa dawa katika vituo vya serikali vya kutolea huduma za afya, masharti magumu ya vibali vya ujenzi katikati ya mji, uhalifu, matukio ya ubakaji na ulawiti, utitiri wa kodi na mengineyo mengi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment