Tuesday, 29 August 2017

CCM YAWATETEA WASIO NA UWEZO WA KUJENGA MAGHOROFA MJINI IRINGA

Image result for Mji wa Iringa

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Iringa kimekosoa ramani mpya ya mipango miji (Master Plan) ya Manispaa ya Iringa kikisema inawanyima wananchi wa kawaida wenye nyumba katikati ya mji kuzifanyia ukarabati na matengenezo makubwa.

Kwa kuzingatia sheria ya mipango miji na ramani hiyo, eneo hilo la katikati ya mji linatakiwa kujengwa nyumba za ghorofa pale wenye nyumba za zamani wanapoamua kuzifanyia ukarabati mkubwa.

“Ni vugumu sana kwa wananchi wa kawaida kujenga maghorofa kwa msingi huo. Mnapotengeneza sheria hizi, wataalamu wetu ni muhimu mkaangalia na uwezo wa watu,” alisema Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Christopher Magala.

Magala alionesha hofu ya sheria hiyo kwenye kikao cha halmashauri kuu ya CCM ya mkoa wa Iringa iliyoketi hivikaribuni kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Magala alisema wakati wananchi wakilazimishwa kujenga maghorofa katika ya mji huo, miundombinu yake iko vile vile jambo linaloweza kusababisha kero kubwa siku za baadae.

Alitoa wito kwa wananchi wasio na uwezo lakini wana nyumba katikati ya mji kutokubali kuuza nyumba zao kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanakaribisha umasikini.

“Wito wangu kwenu, mkilazimika sana kuitekeleza sheria hiyo, angalieni uwezekano wa kuingia ubia na watu wenye uwezo ili na ninyi muwe sehemu ya umiliki wa maghorofa yatakayojengwa,” alisema.

Awali Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Ritta Kabati aliomba sheria hiyo ya ujenzi wa ghorofa katikati ya mji iangaliwe upya kwasababu imeanza kuwa kero kwa wananchi wengi wanaotaka kufanya ukarabati wa nyumba zao.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alikumbusha uwepo wa ramani hiyo ya mji wa Iringa na akasema ni muhimu ikazingatiwa kama kuna dhamira ya kubadilisha sura ya mji wa Iringa.

Masenza alisema katika kuitekeleza sheria ya mipango miji na ramani hiyo hakuna mwananchi mwenye nyumba ya kawaida katikati ya mji atakayelazimishwa kuondoka.

“Kitakachofanywa na wataalamu ni ushauri tu. Lakini wananchi wakipata fursa ya kuingia ubia na wawekezaji katika maeneo yao, wasisite kufanya hivyo. Hiyo itakuwa na faida kubwa kwao,” alisema..


Reactions:

0 comments:

Post a Comment