Sunday, 27 August 2017

CCM MKOA WA IRINGA YARIDHISHWA UJENZI WA HOSPITALI YA WILAYA KILOLOKAMATI ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa imekiri kuridhishwa na awamu ya kwanza ya ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Kilolo inayotarajiwa kuanza kutoa huduma zake mbalimbali mwakani.

Kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Dk John Mwingira aliiambia kamati hiyo iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza kwamba hadi kukamilika kwake awamu hiyo itatumia zaidi ya Sh Bilioni 4.2.

Alisema awamu ya kwanza ya hospitali hiyo iliyoanza kujengwa mwaka 2011 inahusisha ujenzi wa jengo la mionzi, jengo la kupokelea wagonjwa (OPD), jengo la utawala, jengo la huduma ya mama na mtoto, jengo la maabara na jengo la kulaza wagonjwa.

“Ujenzi wa jengo la upasuaji na chumba cha kuhifadhia maiti haujaanza lakini halmashauri imeshafanya makubaliano na SUMA JKT pindi fedha zitakapoletwa, ujenzi uanze mara moja,” alisema.

Kwa kuzingatia ramani ya wizara ya afya, wanawake, jinsia, wazee na watoto, Dk Mwingira alisema ili kukamilisha miundombinu yote ya hospitali hiyo zaidi ya Sh Bilioni 12 zinahitajika.

“Itakapokamilika hospitali hii inalenga kuhudumia zaidi ya wakazi 230,000 kutokana na kasi ya ongezeko la watu wilayani hapa linalokadiriwa kuwa asilimia 1.7 kwa mwaka,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Asia Abdallah alisema wilaya hiyo itaendelea kushirikisha wadau wake wa ndani na nje kuhakikisha miundombinu yote inayohitajika inakamilika.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza aliipongeza wilaya hiyo kwa hatua waliyofikia katika ujenzi huo akisema hospitali hiyo itaiwezesha kupunguza kiwango cha maambukizi ya VVU/Ukimwi, magonjwa na vifo vya watoto na akina mama wajawazito, kupunguza uhitaji wa rufaa za wagonjwa na kukabiliana na uhitaji mkubwa wa huduma za dharula.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Mkoa wa Iringa, Ephraim Mhekwa alisema; “tutatekeleza wajibu wetu kama wasimamizi wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa kuisukuma serikali kutoa fedha zinazohitajika ili kukamilisha mradi huu kwa wakati.”“Kimsingi tumeridhishwa na maendeleo yake. Dhamira ya chama na serikali yake ni kuona wananchi wanafikiwa na huduma zote muhimu kama tulivyowahidi katika kampeni zetu wakati wa Uchaguzi Mkuu,” alisema Mhekwa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment