Monday, 7 August 2017

BENKI ZA WANANCHI ZAKWEPA KUFUTIWA LESENI ZA BIASHARA HIYO

Image result for mucoba bank plc

BENKI ya Wananchi Mufindi (Mucoba PLC) imeridhia kwa mikono miwili uundwaji wa shirikisho la benki za wananchi nchini ikisema hatua hiyo itazisaidia zisifutiwe leseni ikiwa ni matokeo ya nyingi kati yake kutofikia kiwango cha mtaji kinachotakiwa kisheria.

Kwa mujibu wa sheria zinazosimamia sekta ya fedha, benki hizo zinatakiwa kuwa na mtaji wa Sh Bilioni 2 kila moja ili ziendelee kutoa huduma zake.

Hata hivyo taarifa iliyotolewa kwenye kikao cha dharula cha wanahisa wa benki hiyo na  Meneja Uangalizi wa Mabenki wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Thomas Mongella hivikaribuni inaonesha kiwango hicho cha mtaji kimepanda hadi Sh Bilioni 3.5.

Afisa Mtendaji wa Shirikisho la Benki za Wananchi (Cobat ) Rukwaro Senkoro alisema muundo wa shirikisho hilo utasaidia benki hizo kukua kimtaji na kufikia lengo lililowekwa na BOT la kuzitaka benki hizo katika umoja wao kufikisha mtaji wa Sh Bilioni 20.

Alisema kati ya benki 12 za wananchi nchini ni benki tatu tu zenye mtaji wa Sh Bilioni 2 walizotakiwa kuwa nazo kisheria.

Kwa mazingira hayo, Meneja wa Benki ya Wananchi Mufindi (Mucoba) Benny Mahenge alipongeza hatua ya uanzishwaji wa shirikisho hilo akisema utawanusuru wasifutiwe leseni.

Mahenge alisema pia wana matarajio kwamba shirikisho hilo litawawezesha kulinda amana za wateja wao, kufungua matawi mengi zaidi, na kutoa huduma kupitia mawakala na simu za mikononi na zingine ambazo kwasasa hawazitoi.

Kwa upande wake, meneja uangalizi wa mabenki kutoka BOT, Thomas Mongella alisema kwa siku za usoni BOT ina mpango wa kuhama kutoka katika mfumo wa aina tatu za benki na kuwa na aina mbili ambazo ni Benki za Biashara na Microfinance.

“Sote tunafahamu kuwa tunazo aina tatu za Benki ambazo ni Biashara ambayo mtaji wake ni kuanzia Sh Bilioni 15 na kuendelea, Microfinance Sh Bilioni 5 na benki za wananchi ambazo mtaji wake umeongezwa kutoka Sh Bilioni 2 bilioni hadi Sh Bilioni 3.5,” alisema Mongella.

Kabla ya wanahisa hao kuridhia kujiunga na shirikisho baadhi yao walielezea wasiwasi wao kuwa linaweza kuwa chanzo cha mitaji yao kupotea.

“Tuseme tu kwamba mpango huu tunaukubali lakini ni lazima tuhakikishiwe namna mitaji yetu na haki zetu zitakavyolindwa ndani ya shirikisho,” alisema Alex Kalinga.

Kwa upande wake Moses Masasi alisema pamoja na kuukabari mpango huo ni  muhimu kwa wanahisa kuelimishiwa juu ya namna shirikisho litakavyofanya kazi na kuwezesha benki hizo kuwa na nguvu za pamoja.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment