Thursday, 24 August 2017

ASKOFU MDEGELLA AOMBA WADAU KUSAIDIA KULIPA DENI LA BILIONI 1.8


MWENYEKITI wa Bodi ya Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira tawi la Mbeya, Dk Owdenburg Mdegela amewapigia magoti washarika wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) nchini kote akiwaomba wasaidie kulipa zaidi ya Sh Bilioni 1.8 wanazodaiwa na Benki ya Biashara ya Afrika (CBA).

Akizungumza na wanahabari juzi mjini Iringa, Dk Mdegela ambaye ni Askofu Mstaafu wa KKKT Dayosisi ya Iringa alisema chuo hicho ambacho ni sehemu ya kanisa hilo kipo katika hatari ya kuzama kwa kushitakiwa na kuuziwa mali zake, hatua itakayoitia aibu KKKT.

Alisema ameamua kujilipua na kuomba msaada huo kupitia vyombo vya habari baada ya kuona jitihada na mikutano mingi ya kulipa deni hilo na malimbikizo yake ya riba kwa njia za kawaida za kanisa yakipata vikwazo.

Alisema Desemba, 2013 chuo hicho kilikopa kutoka katika benki hiyo zaidi ya Sh Bilioni 1.6 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala na madarasa ya chuo; mkopo ambao sehemu yake haukutumika kwa kazi iliyokusudiwa.

Bila kutaja majina ya wahusika wa matumizi mabaya ya fedha za mkopo huo, Dk Mdegela alisema baadhi ya wajumbe wa bodi na viongozi wa chuo hicho wanapaswa kubeba lawama na kuchukuliwa hatua za kisheria kutokana na ubadhirifu uliofanywa.

“Tumefanya ukaguzi wa hesabu za mkopo huo mara mbili. KKKT ilifanya ukaguzi wake lakini pia kulikuwa na mkaguzi wa nje. Kwa pamoja wamebaini kuwepo kwa ubadhirifu mkubwa, rushwa na ufisadi” alisema.

Alisema ukaguzi wa awali unaonesha asilimia 45 ya mkopo huo ndiyo iliyotumika kwa kazi iliyokusudiwa huku asilimia 55 iliyobaki ikitumika kwa malengo tofauti na ujenzi uliokusudiwa.

“Suala hili limeshakabidhiwa Polisi na kwa wanasheria ili hatua za kisheria kwa wahusika zichukuliwe. Na kwa taarifa ni kwamba wahusika wanaotuhumiwa kwa ubadhirifu huo wamekwisha simamishwa kazi,” alisema bila kuwataja watuhumiwa hao.

Dk Mdegela ambaye pia ni mwenyekiti wa timu ya maaskofu watatu wa kunusuru chuo hicho (Dk Mdegela, Dk Alex Malasula na Dk Abednego Mshahara)  alisema kwa makubaliano ya kulimaza suala hilo kiungwana, benki hiyo imewataka kulipa Sh Milioni 275 ifikapo mwishoni mwa mwezi huu na kwamba marejesho ya deni hilo yataendelea kufanywa kila mwezi.

“Mahali lilipofika suala hili sio mahali pa  kunyamaza, tunataka kila mlutheri na sharika zake zote nchini zijue kinachoendelea na wachangie kunusuru chuo hicho ili kuliondolea kanisa aibu,” alisema.

Alisema ili kufikia makusanyo hayo kutakuwa na makundi manne, la kwanza litajumuisha watu watakaombwa kuchangia Sh 100,000 na kuendelea, la pili watachangia kati ya Sh 50,000 na Sh 100,000, la tatu kati ya Sh 20,000 na Sh 50,000 na la nne kiasi chochote chini ya Sh 20,000.

Pamoja na mapendekezo hayo alisema, watu wataruhusiwa kuchanga zaidi ya kiwango kinachopendekezwa katika makundi yao kwa kadri watakavyoguswa na jambo hilo alilosema ni tatizo kwa kanisa.

“Lakini pia nitalazimika kukutana na walutheri maarufu ambao ni waajiriwa katika taasisi mbalimbali, wafanyabishara na wanasiasa na wadau wengine wa KKKT nchini,” alisema na kuwataja baadhi yao kuwa ni pamoja na Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei.

Pamoja na kupitisha kapu hilo, alisema wanaendelea kuandaa njia nyingine zitakazosaidia kufikia lengo la makusanyo na marejesho ya deni hilo hadi litakapokwisha.

Dk Mdegella aliwataka wadau hao kuchangia chuo hicho kupitia akaunti maalumu No 108433100028 iliyofunguliwa katika benki hiyo ya CBA kwa ajili ya kukusanya na kulipa deni hilo.

Alisema yote hayo anayafanya kwa niaba ya Mkuu wa Kanisa, Askofu Dk Frederick Shoo na kwa niaba ya askofu wa dayosisi ya Iringa, bodi ya wadhamini ya chuo, baraza la uongozi na maaskofu wenzake na wajumbe waliopewa kazi ya kunusuru chuo hicho.

“Kwa yoyote anayehitaji ufafanuzi zaidi anaweza kuwasiliana wa jinsi ya kukisaidia chuo hicho anaweza kuwasiliana name kupitia simu yangu ya mkononi namba 0754313173,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment