Friday, 21 July 2017

ZAIDI YA BILIONI 32 ZA KODI YA MAJENGO ZAKUSANYWA

IMG_4406

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya Sh bilioni 32.5 ya  kodi ya majengo, kwa mwaka wa fedha 2016/17 kutoka katika Majiji, Miji na Manispaa 30 nchini.

Katika hatua nyingine Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango (Mb) amewapongeza  wamiliki wa vituo vya mafuta waliotii  maagizo ya Serikali, kwa kufunga mashine stahiki za EFDs, akitolea mfano vituo vya PUMA na TOTAL ambavyo vimefunga  mashine hizo kwenye pampu zao zote.

Kisha akawageukia wenye maduka ya vifaa vya ujenzi, vileo na maduka makubwa ‘supermarket’ akiwataka nao watumie mashine hizo za kukusanyia mapato ya Serikali (EFDs) kikamilifu na kutoa risiti kwa wateja wao huku akiwaasa wateja nao kudai risiti wanapofanya manunuzi kulingana na kiwango halisi cha bidhaa wanazonunua.

Akizungumzia makusanyo ya kodi ya majengo, Dk Mpango (Mb) amewaambia waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam kwamba makusanyo hayo ni sawa na asilimia 56 ya lengo lililowekwa Mwaka wa Fedha uliopita la kukusanya shilingi bilioni 58.

Alisema kuwa hatua niyo ni mafanikio makubwa tangu TRA ipewe jukumu la kukusanya kodi hiyo ambapo mwaka wa fedha 2015/2016 katika maeneo hayo, Halmashauri zilikusanya kiasi cha shilingi bilioni 28.3.

 “Toka Oktoba mwaka 2016 hadi Julai 15 mwaka huu TRA imekusanya sh. bil 32.5 na kwamba mapato hayo yanatarajiwa kuongezeka kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi kulipa kodi ya majengo,”alisema Dk Mpango.

Akiwaonya wamiliki wa vituo vya mafuta ambao hawatafunga mashine za EFDs ndani ya siku 14 kama agizo la Rais Dk John Pombe Joseph Magufuli linavyoelekeza, Dk Mpango alisema hatua kali zitachukuliwa kwa wale watakaokaidi agizo hilo la Rais.

Alipiga marufuku wafanyabiashara wanaosingizia mashine za EFDs kuwa mbovu na kuwaonesha wateja wao makaratasi waliyotoa taarifa TRA kwamba mashine zao zilikuwa mbovu kwa kipindi kirefu na kuaigiza Mamlaka ya Mapato Tanzania-TRA, kusimamia jambo hilo ili kuhakikisha kuwa linakoma kabisa.

“TRA mtimize majukumu yenu mliyodhaminiwa na Serikali na kuhakikisha kuwa wafanyabiashara ambao mashine zitakuwa hazitumiki ndani ya saa 48 kwa kisingizio cha kuharibika zifungiwe na wamiliki watozwe faini na kulipa kodi ya Serikali ipasavyo” aliagiza Dk Mpango.

“Serikali ya Awamu ya Tano haijaribiwi, tumeazimia tutafanya kazi kwa niaba ya wanyonge ili nchi yetu iende mbele na kwa hili watusamehe.” Alisisitiza Dk MpangoReactions:

0 comments:

Post a Comment